Thursday, September 29, 2011

UZINDUZI WA SWAHILI FASHION WEEK YA NNE


Mwanzilishi wa Swahili Fashion Week,Mustafa Asanali (kulia) akiwa na Mwakilishi kutoka Baraza la Sanaa (BASATA),Ghonche Matengo mara baada ya uzinduzi rasmi uliofanyika kwenye Hoteli ya Southern Sun Dar es Salam leo.Maonyesho yataanza rasmi 10,11na 12 ya mwezi Novemba kwenye Makumbusho ya Taifa
Timu ya waandaaji wa Swahili Fashion ya nne wakiwa n mwakilishi wa basata

KASEBA NA MANENO WATAMBIANA WAKUMBUSHWA SHERIA


Mabondia Japhert Kaseba (kushoto) na Maneno Osward wakitunishiana misuri walipokutana, Dar es salaam leo kukumbushwa sheria mbalimbali zitakazotumika katika mpambano wao utakaofanyika jumamosi hii katikati ni Katibu, wa Chama cha mchezo wa ngumi kinachosimamia mpambano huo. PST. Anton Lutta. (Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com)
Mabondia wakichangia mada




KOcha MKongwe Habibu Kinyogori akichangia mada zinazohusu sheria za mchezo wa ngumi leo

WALEMAVU WASIIONA WAPATA MSAADA WA KATIBA ZA NUKTA NUNDU ZENYE THAMANI YA TSHS 32 MILIONI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Oliver Mhaiki (kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Sauti ya Wanawake Walemavu Tanzania (SWAUTA) Bi. Modesta Mpelembwa sehemu ya nakala 1,500 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 zenye thamani ya Tshs 32 milioni zilizoandikwa katika maandishi ya nukta nundu ili kuwawezesha walemavu wasioona kuisoma Katiba hiyo. Hafla fupi ya makabidhiano hayo imefanyika Wizarani hapo leo Jumanne, Septemba 27, 2011.
Na Mwandishi Wetu
Katika kuhakikisha kuwa elimu ya Katiba inawafikia wananchi wengi zaidi, leo (Jumanne, Septemba 27, 2011), Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeikabidhi asasi isiyo ya kiserikali ya ‘Sauti ya Wanawake Wenye Ulemavu (SWAUTA)’ nakala 1,500 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika maandishi ya nukta nundu zenye thamani ya zaidi ya Tshs 32 milioni.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi nakala hizo iliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Oliver Mhaiki alisema ni nia ya Serikali kuona kuwa makundi yote ya wananchi wanapata elimu ya Katiba hususan katika kipindi hiki cha mchakato kuandikwa kwa Katiba mpya ya nchi.
“Upatikanaji wa Katiba kwa makundi yote hasa katika kipindi hiki kuelekea kuandikwa kwa Katiba mpya ni muhimu sana,” alisema na kuongeza kuwa umuhimu huo unatokana ukweli kuwa Katiba ndiyo sheria mama na hivyo wananchi wa makundi yote hawana budi kuifahamu na kuielewa ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato muhimu wa kihistoria wa kuandika Katiba nyingine baada ya miaka 50 ya Uhuru.
Bw. Mhaiki aliongeza kuwa kutokana na umuhimu huo, ndiyo maana Serikali kupitia Wizara yake ilipopokea ombi la SWAUTA la kutengenezewa nakala za Katiba katika maandishi ya nukta nundu mwezi Mei mwaka huu haikusita kulifanyia kazi uamuzi uliopelekea kutengenezwa kwa Katiba hizo.
“Tulivyopokea ombi lao (SWAUTA) mwezi Mei mwaka huu tukaanza taratibu za kutafuta fedha na manunuzi ambapo hatimaye Kampuni ya Edpar Coporation Ltd ya jijini Dar es Salaam ilishinda zabuni hiyo baada ya taratibu zote za kisheria kuzingatia,” alifafanua Bw. Mhaiki.
Katibu Mkuu huyo aliwaagiza viongozi wa SWAUTA kuhakikisha kuwa Katiba hizo zinatunzwa ili zidumu na hivyo kutumika na walemavu wengi zaidi.
“Kama nilivyosema gharama ya kutengeneza nakala moja ya Katiba katika nukta nundu ni takribani Tshs 21,000/- wakati Katiba iliyopo katika maandishi ya kawaida ni kama Tshs 3,500/-. Hii ni gharama kubwa na ni lazima tuzitunze ili zinufaishe wenzetu wengi zaidi,” alisema katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo na wawakilishi wa walemavu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa SWAUTA Bi. Modesta Mpelembwa aliishukuru Serikali kwa msaada huo na kuahidi kuwa Katiba hizo zitatunzwa kama inavyotarajiwa na Serikali.
Akizungumzia usambazaji wake, Bi. Mpelembwa alisema Katiba hizo zitasambazwa katika mikoa yote kwa lengo la kuwafikia walemavu wakiwemo wanafunzi na wananchi walemavu wa kawaida
“Katiba hizi zitasambazwa katika asasi zote za walemavu bila ubaguzi wa jinsia, dini, umri wala jiografia ili walemavu waweze kupata elimu hii muhimu,” alisema.
SWAUTA ni asasi isio ya kiserikali ya wanawake yenye Makao Makuu yake jijini Dar es Salaam iliyoanzishwa mwaka 2007 kwa lengo la kuwawezesha na kutetea haki za wanawake hususan wenye ulemavu.

WARATIBU WA CHEFA-EA WATEMBELEA NHIF


Sekretarieti ya Mtandao wa Muungano wa Taasisi zisizo za kiserikali za Mifuko ya Afya ya Jamii Afrika Mashariki (CHEFA-EA) imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa namna inavyosimamia huduma ya Mfuko wa Afya ya Jamiii (CHF) nchini.

Pongezi hizo zimetolewa jijini leo na Mratibu wa mtandao huo Bw. Allen Oginga alipokutana na Uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika ziara fupi iliyofanyika Makao Makuu ya Mfuko huo Kurasini.
Bwana Oginga amesema, Tanzania kupitia NHIF imepiga hatua kubwa kwa kuweka uhusiano wa karibu kati yake na mtandao wa CHEFA-EA, hali iliyodhihirishwa na uamuzi wake wa kutoa ofisi katika Makao Makuu yake kwa ajili ya shughuli za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na zile za Mtandao wa CHF tanzania (TNCHF) ambao ni wanachama wa CHEFA-EA.

Awali, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw Hamisi Mdee aliueleza ujumbe wa Sekretarieti hiyo kuwa Bima ya Afya iko tayari kushirikiana na taasisi mbalimali za kijamii ili kuhakikisha kuwa jamii inapata huduma bora za matibabu kupitia NHIF na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao kwa sasa unasimamiwa na NHIF.

Kuhusu walengwa wa huduma za Bima ya Afya, Bw Mdee amesema makundi mbalimbali yamekuwa yakijumuishwa na hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2011 zaidi ya watanzania milioni 5 walikuwa wanahudumiwa na NHIF kupitia Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa CHEFA-EA Bw Gaston Kikuwi amesema, lengo la ziara hiyo ni kujifunza, kubadilishana mawazo, kujenga mahusiano pamoja na kuitambulisha sekretarieti ya mtandao huo.

Kikuwi amesema ofisi za mtandao huo zimehama kutoka Kampala na kuwa Jijini Arusha kuanzia mwezi Julai, 2011 na kwamba uzinduzi wake utafanyika kati ya mwezi Novemba na Desemba mwaka huu.

Mipango ya baadaye ya CHEFA-EA ni kuongeza uwigo wa wanachama washiriki ili kujumuisha nchi zote ziolizoko kwenye shirikisho la ukanda wa Jumuiya ya ushirikiano wa nchi za afrika mashariki.

CHEFA-EA ilianza shughuli zake mwaka 1998 kama jukwaa la majadiliano na baadaye kuwa Mtandao kamili mwaka 2001. Kwa sasa Tanzania, Uganda na Kenya ni wanachama wa mtandao huo.
Wakiwa kwenye Picha ya pamoja baada ya Mkutano kutoka kushoto ni Bi.Penina Odhiambo,Allan Oginga waratibu (CHEFA-EA) kutoka Nairobi-Kenya ,Bwn. Hamis Mdee Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF,kidani Magwila Mratibu wa CHEFA-EA Tanzania,Bwn Rehan Athuman Afisa anayeshughulika na Mifuko ya Afya ya Jamii (CHF),Sister Rita mratibu wa CHEFA-EA Tanzania ,Dr.Mathias Sweya Meneja Miradi ya Afya wa NHIF,Dr.Lawrence Lekashingo,na Mwenyekiti wa VIBINDO na CHEFA-EA Bwn. Gaston kikuwi.

AIRTEL YASAIDIA SHULE ZA SEKONDARI TANGA


Kampuni ya simu ya mkononi ya Airtel kupitia mpango wake wa Airtel shule yetu imetoa msaawa vitabu vyenye thamani ya shilingi milion nne kwa shule za sekondani za mkoani Tanga.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Afisa Biashara wa Airtel mkoani Tanga John Nada amesema kampuni ya airtel kwa kutambua umuhimu wa kuendeleza elimu nchini inatumia sehemu ya faida inayopata na kuirudisha kwa watanzania ili kuboresha huduma za kijamii ambapo hadi sasa imeshatumia zaidi ya shilingi bilion moja kusaidia kuboresha elimu katika nyanja mbalimbali hapa nchini.

Shule zinazofaidika na msaada huu hapa mkoni Tanga ni Tanga Technical Sekondari iliyoko Makorora, Old Tanga iliyopo Tanga mjini, Pande sekondari, iliyoko pande njia ya kuelekea Horohoro pamoja na Toledo sekondari iliyoko maeneo Gofu.

Gharama ya vitabu tunavyokabidhi kwa ujumla vinathamani ya shilingi milioni moja kila shule, na vitabu wanavyopata kila shule ni vtabu vya kiada vya English, sayansi, fizikia, na Hesabati, Lengo letu ni kusaidiana na serikali kuinua kiwango cha elimu ya kila mkoa na dio maana tunatoa msaada huu kwenye mikoa yote.

Akziungumza wakati wa kupokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Tanga Dr.Ibrahimu Msengi aliishukuru airtel pamoja na kuwasisitiza wanafunzi wa shule zote zilizofaidika kuvitumia vitabu kikamilifu ili kujiendeleza kwa manufaa ya jamii zao pamoja na taifa kwa ujumla.

“Msaada wa Airtel wa Vitabu umekuja wakati shule nyingi za sekondari mkoani Tanga zikikabiliwa na upungufu wa vitabu, hivyo hii itasaidia wanafunzi katika kupata maarifa zaidi kwenye masomo”.

Sasa ni jukumu lenu wanafunzi kutumia fursa hii kusoma kwa bidii ili muweze kusaidia taifa baada ya kisomo chenu, msaada huu mkiutumia vizuri ni nyenzo kubwa sana yakusaidia hata faimilia zenu kutokana na faida kubwa mtakayopata kutokana na zao la elimu” alimaliza kusema Dr. Msemi.

Wakipokea msaada huo walimu na wanafunzi wa shule za hizo za sekondari Old Tanga,Tanga Technical, Pande na Toledo wamepongeza mpango wa kampuni ya simu Airtel kuwekeza katika elimu na kuomba makampuni mengine kuona umuhimu wa kusaidia katika sekta ya elimu.

Akiongea kwa Niaba ya walimu wakuu wa shule zilizofaidika na mpango wa Airtel shule yetu Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Old Tanga Kavumo Juma Mzirai alisema “ tunawashukuru sana kwa msaada huu wa vitabu ambavyo tunaamini vitatusaidia kuongeza tija katika ufanisi wa kazi zetu pamoja na kusaidia kuboresha kiwango cha taaluma kwa wanafunzi tunaowafundishia”

Akitoa mfano kuonyesha kiwango cha upungufu ya vifaa vya kufundishia alieleza “Mfano shule ya Old Tanga sekondari inajumla ya wanafunzi wapatao 1,050 ambapo upungufu wa vitabu kwa sasa kuna uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi sita hivyo msaada huu ni dhahiri utapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo tulilo nalo pamoja na kuturahisishia kazi sisi waalimu.

Kampuni ya simu ya Airtel imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia sekta ya elimu kupitia mpango wake wa Airtel Shule Yetu bado inasaidia shule mbali mbali za sekondari hapa nchini kutatua changamoto mbalimbali zikiwemo za vifaa vya kufundisha pamoja na ukarabati wa majengo ya shule hizo kwa lengo la kusaidiana na serikali kutimiza dhamira ya kuinua kiwango cha elimu kila mahali.

Tuesday, September 27, 2011

MBWANA ,MIYAYUSHO WATAMBULISHA MPAMBANO WAO

Bondia Fransic Miyayusho (kushoto) naMbwana Matumla kulia wakitunishiana misuli wakati wa utambulisho wa mpambano wao wa ubingwa wa Mabara (UBO) Dar es Salaam , utakaofanyika mwishoni mwa mezi ujao katikati ni mratibu, Mohamed Bawazir.



MABONDIA WA KINONDONI
MABONDIA WA TEMEKE

Bondia Mbwana Matumla (kushoto) na Fransic Miyayusho kulia wakitunishiana misuli wakati wa utambulisho wa mpambano wao wa ubingwa wa Mabara (UBO) Dar es Salaam , utakaofanyika mwishoni mwa mezi ujao katikati ni mratibu, Mohamed Bawazir.

TUSKER MALT LAGER YADHAMINI TAFRIJA YA HISANI YA SHEAR KIASI CHA SH. MIL25


TUSKER MALT LAGER YADHAMINI TAFRIJA YA HISANI YA SHEAR
(Shear Charity Ball 2011)YENYE LENGO LA KUSAIDIA MRADI WA FISTULA KATIKA HOSPITALI YA CCBRT NA PIA KUWEZESHA KUKARABATI MFUMO WA MAJI KATIKA HOSPITALI YA AMANA
Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ShearIllusions Shekha Nasser ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tafrija ya Shear Charity Ball 2011, katikati ni Ofisa wa Mahusiano ya Jamii Kampuni ya Bia Serengeti (SBL), Nandi Mwiyombela na Ofisa wa Idara ya Mambo ya Ndani SBL Imani Lwinga wakizungumza na waandishi leo asubuhi katika ofisi zao zilizopo Oysterbay Dar es Salaam.
KAMPUNI ya Bia ya Serengeti imetangaza kutoa udhamini mnono kwa katika kuchangia na kufanikisha tafrija ya ‘Shear Charity Ball 2011’ itakayofanyika Jumamosi Oktoba mosi katika hoteli ya Movenpick, Dar es Salaam.
Akitangaza udhamini huo Meneja wa Mahusiano ya Jamii Kampuni ya Bia Serengeti Nandi Mwiyombela alisema.
“Kampuni ya Bia Serengeti ambao ndiyo wadhamini wakuu tuna kila sababu ya jivunia kutangaza kuwa tumechangia kiasi cha sh. mil 25 katika kufanikisha tafrija hii ambayo itaenda sambamba na chakula cha usiku pamoja muziki” alisema .
Alisema tafrija hii itaanza saa moja kamili jioni
Huku wageni walikwa wakiwa wametakiwa kuvaa katika mavazi yenye rangi nyeupe na nyeusi.
“Katika tafrija ya mwaka huu ambayo inafanyika kwa mara ya pili sasa imelenga kuchangisha kiasi cha sh.mil 50 kwa ajili ya taasisi mbili ambazo ni CCBRT na Hospitali ya Amana”alisema Mwiyombela.

Wakati huohuo Mwiyombela aliongeza kwa kusema kuwa leo wasanii wa kundi la Mutati kutoka nchini Kenya watawasili nchini ambapo watatoa burudani katika tafrija hiyo.

“Kesho usiku kutakuwa na muziki katika ukumbi wa Nyumbani Lounge na kiingilio kitakuwa sh.10,000 napenda kuwaeleza kwamba fedha hizo zitapelekwa katika kuchangia matibabu ya upasuaji kwa wagonjwa wa Fistula katika hospitali ya CCBRT na kuweka mfumo wa maji safi na taka Amana
” alisema .

MDAU CARTHBET KAJUNA NA ESTER ULAYA WAMEREMETAA!


MDAU MWANDAMIZI WA BLOG HII CUTHBET KAJUNA KULIA AKIWA NA TABASAMU PANA NA LENYE MATUMAINI YA KUISHI MAISHA YA UPENDO NA MKE WAKE ESTER ULAYA , HAPA NI MARA BAADA YA KUFUNGA PINGU ZA MAISHA JANA, NA KUFUATIWA NA MNUSO WA KUKATA NA MUNDU ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA MBEZI GARDEN , MBEZI BEACH DAR ES SALAAM.


Sisi ni mwili mmoja kuanzia sasa.
Bibi harusi akipongezwa.
Mpambe wa Bwana Harusi Jackson Mbando ambaye pia ni Ofisa Habari wa Kampuni ya simu Airtel akimpongeza Bibi harusi Ester Ulaya mara baada ya kufunga ndoa na kuwa mke halali wa Cuthbet.
Bibi Harusi Ester Ulaya akimwaga tabasamu pama baada ya kuwa mke wa halali wa Cuthbet.
Mmtuonaa eeenhh.
Raha Iliyoje hapa Kajuna Son akiwa na mke wake pamoja na wapambe katika picha ya pamoja.

CUF WALIA KUFUATWA FUATWA NA CHADEMA KWENYE MIKUTANO YAO YA KAMPENI IGUNGA


NA MWANDISHI WETU, IGUNGA
Ntatiro na Magdalena Sakaya wakizungumza leo Igunga

Chama Cha Wanachi (CUF) kimewakemea CHADEMA na kuwataka kuacha siasa za vurugu na kuwafuata fuata kwenye mikutano yao ya kampeni.
Hayo yalisemwa LEO na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Ntatilo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Igunga.
Alisema katika kudhihirisha kuwa CHADEMA ni makamanda wa siasa za vurugu na fujo, wamekuwa wa wakiwafuata fuata CUF kwenye mikutano yao mbalimbali ya kampeni jambo ambalo amesema linakera mno na ni ishaara ya kutafuta maafa.
"Ipo mifano ya wazi kwa hawa CHADEMA kutufutana fuata, kila tunakokuwa na mikutano wanakwenda na gari lao na kuliegesha karibu kabisa na mahali tulipo, haya yalitokea pale Itumba, Nanga na mahali pengi zaidi ya mara nne", alisema Ntatilo.
"Juzi nikiwa na mkutano pale Nanga , watu wawili wakiwa na magwanda ya CHADEMA walikuja na kuingia kabisa kwenye mkutano wetu, eti wakajidai kunisalimia. Hebu niambieni watu wakivaa sare za chama kingine kama CUF au CCM wakiingia mkutano wa CHADEMA wanaweza kusalimika?" aliuliza Ntatilo.
Alisema, baada ya kujidai kumsalimia kwenye mkutano huo, Ntatilo aliwafukuza kistaarabu na kuwataka wasirudie tena utaratibu wao huo mbaya na wa kichokozi.
"Naomba sana katika siku hizi chache zilizobaki CHADEMA wajaribu kuwa wastaarabu ingawa naamini hawawezi, hizo fedha zao wanazogawa wagawe huko huko, wananchi wa Igunga wanachotaka ni uchaguzi wa amani na utulivu siyo magomvi", alisema Mtatilo.
Alisema, vyama vitakavyoendeleza vurugu wakati wa uchaguzi vitakuwa vimechuma dhambi kubwa, kwa sababu baada ya uchaguzi inatakiwa abaki mbunge siyo kuwaachia vifo wananchi wa Igunga.
Kuhusu CHADEMA kuwaita CUF CCM B, Ntatilo alisema, tuhuma hizo ni za kitoto na dalili kwamba CHADEMA hawajui siasa za kistaarab.
" Sisi tulikuwa chama cha vurugu hakuna asiyejua, lakini imefika mahali tukaona kwamba hatuwezi kuendelea kuwa chama cha upinzani tu, lakini lazima tushike dola, sasa tumepata fursa tumepata pale Zanzibar, badala ya kutupongeza hawa CHADEMA wanatukejeli, hawa wanaakili kweli?" alisena Ntatilo.
"Yaani walitaka hata baada ya kufikia maelewano kwamba kuwepo na serikali ya Kitaifa, basi tukatae kila kitu na kuendelea kuwa ngangari tuuuu' ahhh' haiwezekani hicho kitakuwa ni chama kilichokuwa na lengo baya kwa nchi si CUF", alisema.
Katika hatua nyingine Ntatilo ameshusha tuhuma kwa CCM kwamba imeingiza 'janjawidi' kwa ajili ya kufanya fujo wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii.
Hata hivyo CCM imekanusha vikali na kusema kwamba, haiwezi kufanya hivyo, na kwaamba vijana waliopo ni kwa ajili ya kulinda usalama wa viongozi na wanachama wa CCM na vijana hao siyo siri wanajulikana.
Mratibu wa kampeni za CCM, Mwigulu Nchemba alisema, ili kujiweka tayari na kuhakikisha inao vijana wa kutosha katika kusimamia baadhi ya shughuli kama za uwakala wakati wa uchaguzi imewap[a mafunzo ya kikakamavu na ya kujenga akili na siyo ya kijeshi kama inavyopotoshwa.
Wakati huohuo, Katibu wa NEC, Oganaizesheni CCM, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Asha Abdallah Juma, amewataka viongozi wote wa CCM kuhakikisha hakuna mwana-CCM anajitokeza kupiga kura Jumapili.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni za CCM kwenye kijiji cha Ipumbulya,Kata ya Bukoko jimboni hapa, Asha alisema, kimsingi CCM inao wanachama wengi na hata mikutano ya kampeni imedhihirisha hilo kwa hiyo hakuna sababu itakayoifanya CCM ishindwe wanachana, wapenzi na wakereketwa wote watajitokeza kupiga kura.
Asha alisema, serikali ya Chama Cha Mapinduzi itahakikisha unakuwepo usalama wa kutosha katika maeneo yote tangu majumbani, njiani na kwenye vituo vya kupiga kura hivyo mtu yeyote asihofu kutoka akidhani yupo atakayemdhuru.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Steven Wasira amesema hakuna chama chochote cha Siasa ambacho kimeweza kuonyesha hadi sasa kuwa kinaweza kuwa mbadala kwa CCM.
Akimnadi mgombea ubunge wa Igunga kwa tiketi ya CCM, Dk. Dalaly Kafumu, Wasira ambaye ni Mbunge wa Bunda alisema, ni kosa kwa sasa mtu yeyote kudhani kuwa kipo chama chenye uwezo kama CCM katika kuongoza wananchi kwa kuwa havijawa na sera makini.
"Vyama hivi vikija hapa mwanzo wa mkutano hadi mwisho ni matusi weee mpaka basi, na wakijaribu kutoa sera wanakopi zile zile za CCM ambazo wao hawawezi kuzitekeleza kwa kuwa hazi

BAADHI YA MATUKIO MDAHALO WA WAGOMBEA UBUNGE IGUNGA


Wagombea Ubunge jimbo la Igunga, Dk Dalaly Kafumu -CCM (kijanai), Joseph Kashindye -CHADEMA (kaki) na Leopold Mahona-CUF (Bluu) wakipongezana baada ya mdahalo wao uliofanyika usiku wa kuamkia leo mjini Igunga.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Julius Ntatiro, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Mwigulu Nchemba na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zitto Kabwe wakiwa kwenye mdahalo huo.
Polisi akiwatuliza watu wenye munkari waliotaka kuvuruga mdahalo huo kabla ya kuanza
Zitto Kabwe akimvuta mkono Mbunge wa Tabora mjini, Alhaj Aden Rage kumpeleka safu ya mbele kutoka nyuma alikokuwa amekaa. Aliamua kumhamisha baada ya kufanyiwa zogo mara kwa mara ya wafuasi wa CHADEMA
Wagombea wakisubiri kujibu maswali wakati wa mdahalo huo

YOHANA ROBART KUTETEA UBINGWA WAKE



BINGWA wa mkanda wa TPBO Yohana Robert amechezea kichapo kutoka kwa Jonas Godfrey katika pambano lake la maandalizi la kutetea ubingwa huo lililofanyika juzi katika ukumbi wa DDC Magomeni Dar es Salaam.

Kutokana na kichapo hicho Robert atakuwa amejipunguzia heshima ya kutetea ubingwa huo ambao anatarajia kuutetea Septemba 30 mwaka huu jijini Tanga kwa kutwangana na bondia Alan Kamote.

Awali Robert alitakiwa kutwangana na Mohamed Shaaban ambaye hakutokea siku ya kupima uzito hivyo kumfanya Robert kubadilishiwa mpinzani katika dakika za mwisho.

Akizungumzia kichapo hicho Kocha wa Robert, Rajab Mhamila alisema kitendo cha bondia wake kubadilishiwa mpinzani ndicho kilichopelekea kichapo kwa bondia wake.

"Mimi sijafurahishwa kabisa bondia wangu kupigwa kwa sababu imempunguzia heshima ya ubingwa wake pia kitendo cha Shaaban kuingia mitini nacho pia kimenikera kwa kuwa tulitegemea ndiye bondia atakayecheza nae,"alisema Mhamila.

Alisema hata hivyo mapungufu yaliyojitokeza kwa bondia wake atayafanyia kazi ili aweze kufanikiwa kuutetea mkanda huo jijini Tanga.

Bondia Robert alipigwa na Godfrey kwa pointi 40-39 ambapo pambano lao lilikuwa la raundi sita. aliongeza kuwa atatumia nafasi ya kumpereka bondia wake tanga na kuamasisha mchezo wa ngumi kupitia DVD zake za Super D Boxing Coach zinazoelekeza mafunzo ya mchezo huo

TBL YATOA VIFAA VYA MIL 10 WIKI YA USALAMA BARABARANI


Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Mohamed Mpinga (kushoto) akimshukuru Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Steve Kilindo baada ya kupatiwa na TBL msaada wa fulana na kofia vyenye thamani ya sh. mil. 10 kwa ajili ya maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama yatakayofanyika mkoani Kagera kuanzia Oktoba 3-8, mwaka huu. Hafla hiyo ilifanyika Dar es Salaam juzi.
http://fullshangwe.blogspot.com/

MKUU WA MKOA WA RUKWA AWAHAMASISHA WATANZANIA KUWEKEZA NA KUTOWAOGOPA WAGENI WA NJE YA NCHI


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Mayanyanya akizun gumza na waandishi wa habari leo kwenye ukumbi wa Idara ya habari Dar es salaam wakati alipozungumzia Kongamano la Owekezaji litakalofanyika mjini Mpanda Mkoani Rukwa, kushoto ni Katibu tawala wa mkoa huo Salim Muhamed Chima.
Mkuu wa mkoa Mhandisi Stella Manyanya akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wengine kutoka mkioa ya Rukwa, Kigoma na Katavi pamoja na maofisa kutoka kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo leo.

Na Ismail Ngayonga

Maelezo

Dar es Salaam

WATANZANIA na wadau wa maendeleo nchini wamehimizwa kujitokeza na kuwekeza katika vivutio vilivyopo badala ya fursa hizo kuwaachia wageni kutoka nje ya nchi.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano wa uwekezaji katika ukanda wa ziwa Tanganyika unaotajiwa kufanyika tarehe 17 oktoba mwaka huu.

Mhandisi Manyanya alisema wakati umefika kwa Watanzania kujitokeza na kuwa vinara katika sekta ya uwekezaji na kamwe wasitishwe na suala la uwezo, kwani katika mipango iliyopo inawasaidia pia wenye uwezo mdogo wa kuwekeza.

“Mikoa iliyopo katika ukanda wa ziwa Tanganyika ambayo ni Kigoma, Rukwa na Katavi ina fursa nyingi za uwekezaji, hivyo kila Mtanzania anahimizwa kuwekeza hata kama ana uwezo mdogo kifedha yapo baadhi ya maeneo unayoweza kuwekeza” Alisema Mhandisi Manyanya.

Alisema mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ni miongoni mwa mikoa yenye umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi, hivyo katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wa ukanda huo wadau wote wa ndani na nje ya nchi wana fursa sawa ya uwekezaji kupitia mipango iliyopo.

Manyanya alisema kwa muda mrefu ukanda wa ziwa Tanganyika tangu enzi ya ukoloni umesifika kwa miundombinu duni ya huduma za kiuchumi na kijamii, hatua hiyo iliyosababisha mikoa yake kusahaulika katika harakati za maendeleo ya mawasiliano ya barabara, usafiri wa majini, reli, usafiri wa ndege pamoja na mawasiliano ya simu, runinga na redio.

Aliongeza kwa kutambua changamoto hizo, Serikali ya awamu ya nne imefanya kazi kubwa katika kufungua ukanda huo kwa kujenga miundombinu ya barabara za lami, viwanja vya ndege, bandari katika ziwa Tanganyika, upatikanaji wa umeme wa uhakika, pamoja na kuboresha huduma za jamii.

Kwa mujibu wa wa Mhandisi Manyanya alisema kutokana na mabadiliko hayo yaliyofanyika katika ukanda huo, ni fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuingia katika mikoa hiyo ili kuwekeza na hatimaye kuharakisha maendeleo ya wananchi.

“Wawekezaji wenye uzoefu wa biashara za hoteli za kitalii wanakaribishwa kujenga hoteli katika miji ya Kigoma, Mpanda, Sumbawanga, Mwambao mwa ziwa Tanganyika; pamoja na ujenzi wa mahoteli katika mbugas za hifadhi ya katavi, mahale na Gombe” alisema Manyanya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), Bi. Beatrice Chonjo alisema katika kuchagiza mkutano huo, TIC imezihamisha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika mkutano huo, kwani nafasi waliyonayo ni kubwa katika kuharakisha maendeleo ya mikoa ya ukanda huo na taifa kwa ujumla.

Waliosoma Kusini waaswa kuchangia elimu

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Jimbo la Lindi Mjini, Salum Baruany amewashauri watu waliowahi kusoma katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania kushirikiana katika kufanikisha tamasha la kuchangia maendeleo ya elimu kwa ajili ya mikoa hiyo.

Baruany aliyasema hayo juzi katika kikao cha maandalizi ya tamasha la kuchangia maendeleo ya elimu kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kilichofanyika Ukumbi wa Imasco, Temeke jijini Dar es Salaam.

Akiwa mmoja wa waalikwa wa vikao hivyo vya kila wiki, Baruany alielezea kukunwa kwake na ubunifu wa baadhi ya wanafunzi walioamua kuwahamasisha wenzao kukumbuka walikotoka kielimu, kwa lengo la kuwainua wengine.

“Nawapongeza sana. Ni wachache wanaoweza kukumbuka walikotoka, hasa kielimu. Hapa mmelenga, mikoa ya kusini iko nyuma kielimu, naamini wa kusaidia kupandisha hadhi ni ninyi wenyewe mliosoma kule na wadau wengine wanaoguswa na suala hili.

“Msikate tamaa, mtafanikiwa. Cha msingi ni kuwashirikisha na kuwashawishi wengine waliosoma ana kuwa karibu na mazingira ya kielimu ya mikoa hii. Nchi hujengwa na wananchi wenye moyo, nanyi kwa kuguswa kwenu, naamini elimu ya kusini itainuka kwa sababu ni vigumu mtu mmoja mmoja kuchangia na bado maendeleo ya kweli yakaonekana, bali kupitia mshikamano kama wenu,” alisema mbunge huyo.

Naye Mratibu wa tamasha hilo, Asanterabbi Mtaki, licha ya kumshukuru mbunge huyo kwa nasaha zake, aliwataka wadau wa elimu nchini kuungana na waliosoma mikoa ya kusini ili kufanikisha azma ya kuiinua kusini kielimu.

“Tangu awali tumeelezea hali ya elimu ya mikoa ya Kusini, kwa kweli si nzuri na inahitajika nguvu ya ziada, ndiyo maana tumeungana kuhakikisha tunafanikisha kitu kwa ajili ya shule za kusini na wanafunzi wake, hasa yatima, walemavu na wasiojiweza ili wapate haki ya kupata elimu bora,” alisema Mtaki.

Alisisitiza kuwa, kasi ya maandalizi ya tamasha hilo inaridhisha na kuongeza kuwa, nafasi ya waliosoma kusini kuchangia mawazo bado ipo, hasa kupitia vikao vya kila mwisho wa wiki vinavyofanyika ukumbi wa Imasco.

DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL ATOA MHADHARA KUHUSU CHANGAMOTO ZA SAYANSI NCHINI TANZANIA UPPSALA, SWEDEN


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipokea zawadi kutoka kwa Mrembo Miss Africa Scandnavia 2010/2011, Michelle Jeng, baada ya kumalizika kwa mkutano baina yake na Watanzania waishio nchini Sweden, uliofanyika kwenye Ukumbu wa Hoteli ya Gillet Clarion, iliyopo Uppsala nchini hapa jana Septemba 25. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Muhammed Mwinyi Mzale. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipokea zawadi kutoka kwa Mrembo Miss Africa Scandnavia 2010/2011, Michelle Jeng, baada ya kumalizika kwa mkutano baina yake na Watanzania waishio nchini Sweden, uliofanyika kwenye Ukumbu wa Hoteli ya Gillet Clarion, iliyopo Uppsala nchini hapa jana Septemba 25. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Muhammed Mwinyi Mzale. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Na Boniphace Makene
Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ametoa mhadhara kuhusu changamoto za kisayansi katika maadhimisho ya miaka 50 ya Idara ya Sayansi za Kimataifa kwa kifupi ISP ya Chuo Kikuu cha Uppsala kilichopo Uswidi ambapo amefafanua kuwa, mchango wa wanasayansi kutoka katika chuo hiki una manufaa makubwa katika kukuza teknolojia katika sayansi kwa nchi za Afrika.
Makamu wa Rais ambaye alikuwa mhadhiri wa somo la Fizikia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kabla ya kuingia katika siasa, amealikwa na wanasayansi wa kariba yake katika maadhimisho haya yaliyo na lengo la kutanua uwanda wa tafiti katika nchi za Afrika na hasa Tanzania, ambayo kwa sasa imeanzisha chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo Arusha.
Katika ziara hii ambayo Makamu wa Rais ameambatana na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Telezya Huvisa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim pamoja na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela Profesa Burton Mwamilwa.
Ujumbe wa Makamu wa Rais ulifika hapa na kupata nafasi ya kuzungumza na Watanzania waliopo Uppsala ambao wengi walitaka kujua kama Tanzania imejipanga vema kukabiliana na tatizo la umeme nchini. Makamu wa Rais ambaye katika ziara hii amekuwa akikutana na wanasayansi mbalimbali wa Sweden na hasa waliobobea katika sekta ya nishati aliwaeleza Watanzania waliokuwa katika mkutano naye kuwa; kama taifa tuna kila sababu ya kukubali kuwa tulifanya makosa huko nyuma kwa kutotambua utanuaji wa vyanzo vya umeme wa uhakika hali inayotuumiza sasa lakini pia akawaambia kuwa serikali imejipanga vema kuhakikisha kuwa tatizo la umeme linapata tiba katika kipindi kifupi na pia kuwa na umeme wa uhakika katika miaka miwili ijayo.
Maeneo makubwa ambayo Makamu wa Rais amekuwa akiwasikiliza kwa ukaribu wanasayansi wa Uppsala na Sweden ni kuhusu vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa umeme vikiwemo vile vya upepo na maji ya bahari huku pia ikiwa Tanzania imeshasaini mkataba wa uzalishaji wa umeme wa makaa yam awe na kampuni ya kutoka China, mkataba uliosainiwa wiki mbili zilizopita katika ya NDC na kampuni ya China ambazo zitashirikiana katika miradi mikubwa katika ukanda wa Mtwara.
Eneo jingine ambalo Makamu wa Rais amekuja kulihamasisha ni juu ya uhusiano wa chuo hiki kikongwe katika uwanja wa Sayansi na namna chuo hiki kitakavyozidisha ushirikiano wake katika kusomesha wataalamu wa Tanzania katika ngazi za Shahada za Uzamivu na mchango mkubwa ukiwa kukipatia uwezo Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela kilichopo Arusha.
Katika ziara hii ya kitaaluma aliyoalikwa Makamu wa Rais inayochukua siku mbili, Makamu wa Rais pia atakutana na Waziri wa Mambo ya Jamii wa Uswidi Ulf Kristersson na Waziri wa Mahusiano na Maendeleo Gunilla Carlsson. Katika ratiba hiyo pia Makamu wa Rais atatembelea Taasisi ya Mazingira ya Uswidi sambamba na kuzungumzia mafanikio ya Kilimo Kwanza kwa wadau wa maendeleo wa Uswidi.

Mgombea Ubunge anapojipumzisha kwa kucheza pool table



Mgombea Ubunge Jimbo la Igunga kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Leopold Mahona akishiriki kucheza mchezo wa pool table katika mji wa Nkinga wilayani Igunga.