Sunday, May 30, 2010
CCM WAINGIA KULINDA MAJIMBO YAO
Waziri Mwakyusa na mbunge Kilasi kuhojiwa na Takukuru kwa kumwaga fedha majimboni mwao
Thobiass Mwanakatwe
Na Thobias Mwanakatwe, Mbeya
SAKATA la Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Prof.David Mwakyusa na Mbunge wa Mbarali, Esterina Kilasi, wanaodaiwa kumwaga fedha na baiskeli katika majimbo yao katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu sasa limetinga katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) Mkoa wa Mbeya ambayo imeanza kuchunguza masuala hayo.
Pro.Mwakyusa ambaye ni Mbunge wa Rungwe Magharibi kati ya mwezi Marchi na April mwaka huu alitoa Sh.500,000 kila kata katika kata 19 za jimbo lake kwa madai zisaidie kuimarisha chama hali iliyozua mjadala mzito kutoka kwa wananchi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Rungwe.
Awali fedha hizo alizikabidhi kwa viongozi wa chama wa kata husika wakati akiwa katika ziara jimboni mwake ambapo alitoa kwa kata 10 na baadaye kata nyingine 9 zilizokuwa zimesalia zilikabidhiwa kwa viongozi wa kata katika Ofisi za CCM za Wilaya kazi ambayo ilifanywa na Katibu wa CCM Wilaya ya Rungwe, Daudi Ilanga.
Kwaupande wake Mbunge wa Mbarali, Kilasi katika kipindi cha mwezi huo wa Marchi, anadaiwa kuwamwagia Makatibu wa Siasa na Uenezi wapatao 11 wa jimbo hilo Sh.100,000 kila mmoja ili wazitumie kama nauli ya kwenda Dodoma bungeni kutalii hali ambayo pia ilizua malalamiko kwa wananchi na wanachama wa wilaya hiyo.
Kilasi mbali na kutoa kiasi hicho cha fedha kwa Makatibu wa Siasa na Uenezi, pia aligawa baiskeli kwa Makatibu Kata 11 wa CCM wa jimbo lake ili ziwarahisishie kufanya kazi za chama kwenye kata zao katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Wabunge hao wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti walithibisha kutoa fedha hizo kwa viongozi hao wa chama na kwamba walifanya hivyo kwa kuwa waliomba na pia walikuwa wanatekeleza utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi.
Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya,Respick Ndowo, akizungumza katika mahojiano na Nipashe ofisini kwake jana, alisema taasisi yake baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari na wadau wengine wameanza kuchunguza madai ya wabunge hao wanaodaiwa kumwaga fedha majimboni mwao.
Ndowo alisema mbali na kuchunguza suala hilo, pia TAKUKURU inaendelea na uchunguzi wa madai ya wabunge wa mkoa wa Mbeya waliodai kuwa wapo watu wamemwaga mamilioni ya fedha kwenye majimbo yao kwa ajili ya kuwachafua ili wasiweze kuchaguliwa katika uchaguzi wa mwaka huu.
“TAKUKURU vilevile bado tunaendelea na uchunguzi wa madai yaliyotolewa na baadhi ya wabunge kwamba mafisadi wamemwaga fedha kwenye majimbo yao kwa ajili ya kuwahonga wananchi ili wawachukie na wasiwachague,”alisema Ndowo.
Akizungumza juzi wakati akihojiwa na kipindi cha Power Breakfast cha Radio Clouds FM, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk.Edward Hosea,alisema taasisi yake itawahoji wanasiasa waliotoa pikipiki,baiskeli na zawadi mbalimbali katika majimbo yao.
Dk.Hosea ambaye alikuwa akizungumzia Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010,alisema,pamoja na uchunguzi kufanyika taasisi yake inaendelea kukusanya taarifa na itakuwa makini haitamwonea mtu wala kumsingizia na kusiistiza kuwa haitakurukupuka katika hilo
Alisema watu waliotoa vifaa hivyo vya usafirina vingine orodha yao ipo na wataitwa taratibu na kwa heshima kuhojiwa kujua vyanzo vya mapato yao na atakayeshindwa kujieleza atafikishwa mahakamani.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema inashangaza kuwa kwanini watu hao wapeleke zawadi hizo wakati huu unaokaribia uchaguzi na si wakati mwingine huko nyuma na kwamba wamekuwa wakipeleka vitu hivyo kwa watu mahsusi na si chama.
Alisema kama watu hao walikuwa na lengo la kusaidia vitu hivyo ilipaswa kutolewa mathalani kwa kijiji na isi kwa watu Fulani, hali ambayo inatia shaka kuwa vina lengo la kushinikiza watu hao wampigie kurwa mtu au chama fulani.
Kamanda huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya aliongeza kuwa kitu cha msingi kinachotakiwa kuzingatiwa na wabunge hao ni kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ili kama ni kweli wapo watu waliomwaga fedha majimbo watakapobainika hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mara moja.
Alisema kama wabunge hao wanaona ni vigumu kwao kwenda ofisi za Takukuru zilizopo mkoani na wilayani waende hata kwa Wakuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa au kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wakatoe maelezo ikiwezekana kutaja watu wanaowatuhumu kuhusika na ugawaji wa fedha hizo majimboni mwao.
“Tunawaomba wabunge kama wanaona ni vigumu kwenda kuja katika ofisi zetu za TAKUKURU basi waende hata kwa DC, RC au kwa RPC wakatoe maelezo, lakini hata hivyo hatutegemei mbunge ambaye ndiye anashiriki katika kutunga sheria akatae kuja kuja kutoa ushirikiano kwetu,”alisema Ndowo.
Katika kipindi cha mwishoni mwa mwaka jana na mwaka huu wabunge watatu walitoa maelezo kuwa wapo watu au mafisadi ambao wamemwaga fedha majimbo mwao ili kuwashawishi wananchi wasiweze kuwachagua.
Wabunge hao ni Mbunge wa jimbo la Lupa, Victor Mwambalaswa,Mbunge wa Mbeya Mjini,Bensoy Mpesya na Mbunge wa Kyela, Dk.Harrison Mwakyembe.
No comments:
Post a Comment