Sunday, May 23, 2010

HASHIMU APAISHA MAJUU MCHEZO WA BASKET TANZANIA


HASHIMU AKIFUNGA BASKETI WAKATI WA MICHEZO YAKE

hASHIMU ARIPOFANYA DHIARA TANZNIA

Na Amina Athumani

"NAFANYA mchezo ambao ninaupenda kutoka ndani ya moyo wangu, suala la pesa nalipwa kiasi gani silifuatilii sana, ili mradi kiwango changu kisishuke, nachezea Ligi ya NBA ambayo inaushindani mkubwa sana nchini Marekani,"

"hakuna mchezaji anayeweza kumtegea mchezaji mwenzie ndani ya timu iwe kwenye mazoezi ama mechi ngumu hivyo ninajali sana mazoezi ili kupandisha kiwango changu zaidi kwani nisingependa nirudi tena nyuma zaidi ya kusonga mbele na kuonesha mafanikio zaidi katika kikapu.,"

Maneno hayo yalisemwa na mchezaji wa Tanzania Hashim Thabit anayechezea ligi ya Mpira wa kikapu nchini Marekani (NBA) Katika timu ya Memphis Glizzlies ya nchini humo ambayo inashiriki Ligi hiyo.

Mchezaji huyo kwa sasa ni kioo cha Taifa katika mchezo huo kwani mafanikio yake huenda yakawavutia wachezaji wengi wa nchini ili nao kuweza kutimiza ndoto kama alizozipata mchezaji huyu.

Hashim kwa upande wake anasema ingawa ameweza kupata mafanikio katika mchezo huo, anachoweza kufikiria zaidi ni kuweza kuinua mchezo wa kikapu nchini ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wachezaji wa Tanzania wenye vipaji kuweza kufika mbali.

Mchezaji huyo ambaye anapokea zaidi ya dola elfu 92 kwa wiki ambazo ni sawa na sh. za kitanzania zaidi ya milioni 100, huku akipokea dola milioni 4.4 kwa mwaka, na dola laki 3.7 kwa mwezi katika msimu wa mwaka 20009-2010, anasema kamwe hatabadilika kutokana na pesa, zaidi yeye anafikiria kiwango chake cha mchezo huo kutokana na kwamba anaufanya kwa sababu anaupenda.

Hashim ambaye kwa sasa yupo nchini kwa ajili ya mapunziko ikiwa ni pamoja na kufanya ziara za mchezo huo kwa timu za mpira wa kikapu za hapa nchini, ziara yake imeweza kuwa na mafanikio makubwa sana.

Mafanikio hayo ni pamoja na kutoa changamoto kwa Serikali ambayo awali ilikuwa imegeukia michezo mingine na sasa imeona umuhimu wa kuunganisha nguvu na Shirikisho la mpira wa kikapu ili kuona mafanikio zaidi yanapatikana.

Moja ya changamoto hizo ambazo Serikali inazifanyia kazi ni kuhakikisha inamleta kocha wa kigeni wa kimataifa atakayeweza kuufundisha mchezo huo kwa kiwango cha kimataifa ili kupiga hatua zaidi katika soko hilo.

Kwa kuanza na mpango mkakati wa kuusaidia mchezo huo, Serikali imelipia gharama za waamuzi wawili wa kikapu nchini kwa ajili ya kushiriki kozi ya kimataifa ya mchezo huo itakayofanyika nchini Cameroon.

Waamuzi waliogharamiwa safari hiyo ni pamoja na Gosbert Boniface na Joseph kitundu ambapo kutokana na ziara ya mchezaji huyo ndio iliyosababisha nguvu ya Serikali kuingia katika kusaidia mchezo huo zaidi.

Inawezekana kwamba Serikali ilikuwa na mpango au mawazo ya kusaidia mchezo huo lakini isingekuwa kwa muda huu inawezekana labda ingekuwa kwa baadaye alikini nguvu ya mchezaji huyu imeisukuma Serikali hadi kupelekea kuahidi kufanya mambo makubwa katika mchezo huo.

mbali na changamoto hizo zilizotokana na mchezaji huyo pia mafanikio kwa upande mwingine yalionekana katika ziara hiyo kwa upande wa wachezaji wa mpira wa kikapu ambao ni vijana wa shule za Sekondari.

Wachezaji hawa wameweza kujifunza vitu vingi kutoka kwa mchezaji huyo hasa kwa upande wa kupewa ujasiri wa kujiamini kuwa wanaweza kufanya vizuri, endapo watatilia mkazo Elimu na michezo.

Pia katika suala zima la kuwataka kufanya mazoezi kwa bidii zote ikiwa ni pamoja na kusikiliza maelekezo wanayopewa na walimu wao ambapo anasema siri kubwa ya mafanikio kwa mchezaji ni kufanya mazoezi sana na kupata muda mwingi wa kupunzika.

"Mimi ninafanya mazoezi matatu tofauti kabla ya kujichanganya katika mazoezi ya jumla na wachezaji wenzangu, baada ya kupata chai naingia katika Gym na ninafanya mazoezi magumu kama ya kubeba vyuma na vitu vizito,"

"Baada ya hapo nafanya mazoezi nikiwa na mwalimu wangu ambaye ananielekeza vitu mbalimbali kuhusu mchezo na ninapomalizi ndio naingia kiwanjani kwa ajili ya mazoezo ya uwanjani na baadaye najiunga na timu na tunafanya mazoezi ya jumla,"anasema thabeet

Anasema bila mazoezi kiwango cha mchezaji ni lazima kishuke na kuwashauri vijana hao kujali zaidi mazoezi ikiwa ni pamoja na kuzingatia nidhamu wakiwa ndani na nje ya uwanja.

"Elimu ni moja ya mafanikio kwa mchezaji yoyote ambaye angependa kucheza mpira wa kikapu nchini Marekani katika Ligi ya (NBA), wachezaji wengi wa NBA ni wasomi hivyo nawasihi muzingatie Elimu ili muweze kuwa wachezaji wa kulipwa na wenye mafanikio makubwa sana,".

"Naahidi kuboresha mpira wa kikapu nchini kwa shule za msingi na Sekondari kwa kuwa vipaji halisi vya wanamichezo na wasomi vinaanzia kwa vijana wadogo,"anasema Hashim.

Anasema atakuwa nchini kwa kipindi kifupi kwa ajili ya kuandaa maboresho ya mchezo huo kwa kushirikiana na TBF pamoja na Serikali inayosimamia michezo nchini.

"Tanzania inawatoto wengi wenye vipaji lakini hawajui jinsi ya kuviendeleza kwa sababu hawana msaada kutoka sehemu yoyote, nimegundua kuwa wazazi wengi wanawanyima vijana fursa ya kushiriki michezo, kwa upande wangu ninamshukuru sana mama yangu kwa kunipa sapoti hadi kufikia hapa,"anasema Thabeet.

Anasema maboresho atakayoanza nayo ni katika miundombinu ambapo sasa yupo katika mazungumzo na makampuni mbalimbali ambayo yapo tayari kusaidia.

Anasema ni jukumu sasa la kila mpenda maendeleo ya mchezo huo kwa nafasi yake kuhakikisha anatoa mchango wa ujenzi wa viwanja vya mchezo huo kwa kila mkoa ili iwe rahisi kwa kuchezwa mchezo huo kwa mikoa yote ya Tanzania.

Anasema kwa wachezaji ambao wana uwezo katika viwango vya mchezo huo atawapeleka nchini Marekani na kuwaingiza katika timu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwajenga Kisaikolojia.

"Hata hivyo siwezi kuahidi mambo mengi ila tutaangalia linalowezekana kulifanya ili mradi mungu atupe uzima na salama,"anasema Thabeet.

Kwa upande wa Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na michezo Joel Bendera ambaye alikuwea sambamba na mchezaji huyo katika ziara hiyo anasema anampongeza mchezaji huyo kwa kufikia uwamuzi huo wa kukuza mchezo wa kikapu nchini na kuahidi kuwa Serikali itawekeza nguvu katika mchezo huo ili Tanzania iweze kuwa na wachezaji wengi wenye mfano wa Thabit.

"Pamoja na nguvu za Thabeet alizozionesha katika mchezo wa kikapu Serikali pamoja na Shirikisho la mpira wa kikapu tutasaidiana katika kuboresha miundombini hasa ya viwanja,"anasema Bendera.

Nao TBF, hawakusita kuzungumzia mafanikio yaliyoonekana katika ziara ya mchezaji huyo na kusema, kuwepo kwa Hasheem ni bahati ya pekee kwa watanzania katika kutumia nafasi waliyo nayo na kushirikiana naye kuleta mabadiliko nchini.

"Shirikisho lipo kwa ajili ya maendeleo ya mchezo wa mpira wa kikapu Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wachezaji lakini nguvu iliyooneshwa na mchezaji huyo imeleta matumaini mapya, tutahakikisha tunaunganisha nguvu hizi ili kuleta mapinduzi makubwa ya mchezo huu,"anasema Katibu msaidizi wa TBF, Michael Maluwe.

Anasema Vijana walioweza kufika katika ziara ya Thabeet wamefaidika na mawazo ya Hasheem na jinsi ambavyo aliweza kufanikiwa kucheza NBA sio kitu rahisi na kwamba wamejua kuwa Elimu pia ilichangia kufanikisha malengo yake.

Katibu huyo anasema kwa upande wa mafunzo ya juu ya mchezo huo kwa vijana bado hawajapata ila yale aliyoyaongea Hasheem vijana wanapaswa kuyazigatia na kuyafanyia kazi kwani wanayo nafasi kubwa ya kufanya mambo mazuri hapo baadaye.

Hashimu pia hakusita kuzungumzia ndoto zake za baadaye na kusema kuwa ipo siku atacheza michuano ya Olimpiki ambayo huwakiliusha wachezaji kutoka nchi husika.

Anasema kutokana na nchi yake kukosa fursa ya kucheza michuano hiyo kwa sasa kutokanba na kutokuwa na viwango stahiki, anasema ipo siku Tanzania itacheza michuano hiyo na yeye akiwa mmoja wa wachezaji watakaotetea Taifa lake katika kuleta mafanikio na ushindani.

"Ninaimani ndani ya miaka 10 au 15 ijayo Tanzania itapata nafasi ya kucheza mashindano haya makubwa ila ninawaomba TBF na Serikali kuwekeza nguvu zaidi ili Tanzania iwe moja wa washiriki katika michuano ya Olimpiki ya mwaka 2016,"anasema Thabit.

Thabit anasema ingawa ianacheza NBA Marekani kamwe hataweza kuuza Utanzania wake na kujivua Uraia na kuwa raia wa nchi nyingine, atabaki kuwa mtanzania halisi hata kama atapata mafanikio na vishawishi vya kiasi gani.

"Siwezi kuutupa uraia wangu ingawa nina hamu sana ya kucheza Olimpiki hata inifuate nchi gani ya Afrika iniombe nikawakilishe Taifa lao, nchi ambayo si ya Tanzania kamwe siwezi kukubali.

Hashim anamalizia kwa kusema ingawa yeye ni mwanamichezo pia anategemea kuwa mfanyabiashara na kwamba hizo zote ni moja ya ndoto zake za baadaye

No comments:

Post a Comment