Friday, July 30, 2010
BONDIA BADRU HASSAN ALIVYOUPENDA MCHEZO WA NGUMI
BADRU
BONDIA BADRU AKICHEZA KATIKA MOJA YA MECHI ZAKE
Na Shaban Mbegu
KAMA si mchezo wa masumbwi basi leo hii na mimi ningekuwa ni mmoja kati ya wachezaji wanaowaniwa na klabu mbalimbali za soka kutokana na uwezo wangu wa kumiliki mpira nikiwa kama kiungo na wakati mwingine kucheza sehemu ya ushambuliaji.
Maneno hayo yamesemwa na Badrua Hassan 'Muhindi Mweusi' ambaye ni mmoja wa wanamasumbwi wanaounda klabu mpya ya mchezo ngumi ya Ashanti, ambayo imeonekana kufufua mchezo huo katika wilaya ya Ilala.
Akizungumza na gazeti hili Muhindi Mweusi anasema toka akiwa mdogo ndoto zake zilikuwa ni kuhakikisha anakuwa ni mchezaji tishio katika soka la Tanzania kama ilivyokuwa kwa wachezaji kama Abdallaha Kibadeni, Sunday Kayuni, Madaraka Selemani na Edibili Lunyamila ambao katika historia ya soka ya Tanzania na wao wamo.
"Nakumbuka katika miaka ya 90 niliwahi kusajiliwa na timu ya Oman FC ambako huko sikudumu sana kabla ya kujiunga na Matambo FC ambao nako pia sikuweza kukaa sana kabla ya kuhamia katika timu ya Six Villa nilipoweza kudumu kwa miaka kadhaa", anasema.
"Kutokana na kipaji nilichokuwa nacho nilijikuta nikihamahama kutokana na baadhi ya viongozi wa timu hizo kila walipokuwa wakinishuhudia mchezo wangu niliwavutia, na kutokana na umri wangu kuwa mdogo nilijikuta nikiwa nayumba katika maamuzi yangu na kusababisha kuwa situlii katika timu moja", anasema.
Anasema alijikuta anaachana rasmi na mchezo wa soka baada ya kuhama kutoka Bugurunin walipokuwa wakiishi na wazazi wake na kuhamia Ilala ambapo huko alikutana na vijana wenzake ambao walikuwa wakipenda zaidi mchezo wa masumbwi kuliko soka katika mtaa wao.
Anasema akiwa huko alijiunga na klabu ya mtaani kwao ambayo ilikuwa inaundwa na vijana mbalimbali waliokuwa wikiishi Ilala ambao walikuwa wakifanya mazoezi kila siku jioni na siku za mwishoni mwa wiki walikwenda katika fukwe mbalimbali.
Anasema baada kuanza kuonekana katika mapambano kadhaa ambayo walikuwa wakipanda katika ukumbi wa lango la jiji katika sikukuu mbalimbali kwa ajili ya kuchangisha pesa kwa ajili kutengeneza gym yao ya mazoezi, ambako huko alionekana na kuchuliwa na kocha George Kanuti ambaye kwa sasa ni marehemu.
"Kutokana na uwezo wangu wa kutupa makonde na kukwepa nilimvutia kocha Kanuti na kunichukua kunipeleka katika klabu yake ya Magomeni usalama ambako huko pia niliweza kung'aa kutokana na kushinda mapambano yote sita ya kirafiki niliyopigana kwa nyakati tofauti", anasema.
Anasema kutokana na uwezo wake aliokuwanao katika mchezo huo, kulitokea nafasi za kujinga na Jeshi la Wanachi Tanznia (JWTZ), ambao wao walikuwa wakihitaji mabondia kwa ajili ya kujiunga na jeshi lao.
"Nakumbuka wale viongozi wa jeshi walituona katika michezo ya kirafiki na kutukubali, tulikuwa kama watano hivi, lakini katika hali ya kushangaza mimi nilikataa kujiunga na jeshi na kuamua kukimbilia nchini Afrika Kusini kutafuta maisha", anasema.
Anasema ilipofika mwezi wa tatu mwaka 1999 aliamua kuzamia rasmi kwenda nchini Afrika Kusini kutafuta maisha ambako huko alidumu kwa miaka mitatu kabla ya mwaka 2003 kurudishwa nchini kutokana na kutokuwa na kibali halali cha kuishi nchini humo.
"Maisha ni mzunguko kaka, wakati nipo Ilala nikutana na wenzangu ambao walikuwa na mawazo ya kwenda mbele na kutokana na kuwa nao katika maisha ya kila siku nilijikuta na mimi nikitamani kwenda, nikafanya mpango na kuondoka zangu, ambapo huko pia nilikumbushia kucheza soka katika timu za mitaani na kukubalika", anasema.
Anasema baada ya kurudishwa nchini alijiunga tena katika klabu yake ya Magomeni pamoja na kuanzisha maisha mapya kwa kuanza kufanya biashara ya kuuza mitumba katika soko la Ilala, biashara ambayo anayifanya mpaka hivi sasa kutokana na kuitegemea kama ndio ajira inayoendesha maisha yake.
Anasema lakini mambo yalibadilika baada ya kocha wao George Kanuti kufariki, kitu kilichopelekea nyumba waliyokuwa wakitumia kama gym yao, kupangishwa kwa mtu mwingine na kusababisha kukosa sehenu ya kufanyia mazoezi na klabu hiyo kufa kabisa.
Bondia huyo anayepigana katika uzito wa kilo 55 anasema baada ya kifo cha kocha huyo waliamua kuanzisha ya kwao katika bustani ya maua iliyopo magomeni lakini kutokana na kutokuwa na vifaa walijikuta wakishindwa kudumu na klabu hiyo na kuamua kila mtu kufanya mazoezi kivyake.
"Kutokana na ubora wangu katika mchezo wa musumbwi kuna siku wakati nimemaliza pambano langu katika ukumbi wa DDC Kariakoo, nilikutana na kocha Rajabu Mhamira 'Super D' ambaye alionekana kunikubali na kunieleza nia yake ya kutaka niwe mmoja wa nitakaeunda klabu ya Ashanti", anasema.
Anasema kutokana na kutokuwa na klabu pamoja na kugundua kocha huyo anatokea katika wilaya ya Ilala alimua kukubali bila pingamizi na kujiunga rasmi na klabu hiyo yenye lengo la kufufua mchezo wa masumbwi katika wilaya hiyo.
Akizungumzia klabu yake mpya ya Ashanti anasema kwa kiasi kikukbwa kocha Super D ameweza kumbadilisha kwa kipindi kifupi ambacho wamekuwa pamoja na kuongeza kuwa katika kipindi hicho ameshapigana mapambano matatu ya kirafiki na kushinda yote.
"Naishukuru sana klabu ya Ashanti kwani imeweza kunifanya hivi sasa kujulikana katika medani ya masumbwi kutokana na kunitangaza pamoja na uwezo wa kocha wetu katika kutufundisha pamoja na kututafutia mapambano mbalimbali ya kirafiki ambayo yamezidi kutujenga", anasema.
Muhindi Mweusi pia alitoa shukrani kwa Shirikisho la ngimi za ridhaa nchini (BFT), kutokana na mchango wake kwa klabu hiyo ususani siku ya mapambano mbalimbali yaliyoandaliwa na klabu hiyo katika kuhamasisha mchezo huo ambapo kwa upande wa chama hicho kiliwakilishwa na Katibu Mkuu wake Makore Mashaga.
Bondia huyo pia aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia mchezo huo kama wanavyofanya katika michezo mingine, kwani bado mchezo huo unakabiliwa na changamoto nyingi kama vifaa vya kufanyia mazoezi.
"Tunawaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutupa sapoti ili na sisi tuweze kuitangaza nchini yetu kupitia mchezo wa masumbwi ambao katika miaka ya nyuma ulipata mafanikio kutokana na mabondia kama Rashids Mtumla 'Snake Boy' na Joseph Malwa walivyoweza kuitanga nchi yetu", anasema.
Pia mchezaji huyo aliwataka vijana mbalimbali kuwa na malengo katika maisha ili waweze kupata mafanikio katika maisha yao, ambapo aliongeza kuwa kuliko kukaa vijiweni na kuvuta bangi basi wangekuwa na ratiba za kushiriki katika michezo mbalimbali ambayo katika miaka ya hivi karibuni imetokea kuwa ajira tosha.
"Katika maisha hakuna kitu kinachoshindikana kama kweli wana nia wateweza kupigana na wasiogope kujifunza mchezo huu wa ngumi kwa kuwa ni mchezo wa hatari kwani naamani kila mchezo una ubaya wake na uzuri wake cha msingi ni kuwa makini katika kitu unachokifanya", anasema.
Badru Hassani ambaye ni baba wa mtoto mmoja anayeitwa Yusra, ni mtoto wa mwisho kuzaliwa katika familia ya watoto tisa ya Mzee Hassani ambapo alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Karume, hakuendelea na kusoma kutokana na uwezo mdogo wa wazazi wake.
No comments:
Post a Comment