Wednesday, July 7, 2010
SHY-ROSE BHANJI NAE AJITOSA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA KINONDONI
• Asema mwaka 2010 ubunge unahitaji tafsiri mpya
• Aainisha maeneo nane atayoyafanyia kazi
• Kupiga vita utumiaji wa madawa ya kulevya kwa vijana
• abainisha umuhimu wa ofisi kila kata ndani ya jimbo
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shy-Rose Sadruddin Bhanji ametangaza kujitosa katika nafasi ya ubunge jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam kupitia CCM na lengo lake kubwa ni kuwa kiungo muhimu katika jamii ya wanakinondoni.
Akitangaza azma yake ya kuomba ridhaa kwa wanachama wa CCM katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Shy-Rose alisema kwa mtazamo wake neno ubunge kwa mwaka 2010 linahitaji tafsiri mpya kabisa. `…kwa sasa mbunge anatakiwa kuwa ni kiungo cha jamii badala ya kuwa mwakilishi wa jimbo kama ilivyozoeleka` alifafanua Shy-Rose.
`Mwaka 2010 ni mwaka wa mabadiliko na ndio maana nimeona kwamba ili kila mwananchi kuweza kuwajibika, nafasi ya mbunge inahitaji kutafsiriwa upya ili iendane na wakati na matatizo ambayo yanayotukakabili wananch` alisema.
Kwa maana hiyo amesema kwamba hata sifa za mbunge zinahitaji kutafsiriwa upya kabisa, kwani majukumu yake yamebadilika kuendana na wakati. Ametaja baadhi ya sifa hizo mpya ni kuwa mhamasishaji, kiungo muhimu, kufanya kazi usiku na mchana na kuwa na ofisi katika kila kata ndani ya jimbo husika ili kuwafikia wananchi kwa ukaribu zaidi.
`naomba nitoe tafsiri mpya ya neno ubunge..mbunge anatakiwa sasa awe ni kiungo muhimu kati ya walio na kipato kikubwa, kipato cha kati na wasio na kipato kabisa ili kwa pamoja jimbo liweze kupiga hatua za kimaendeleo. Mimi nitahakikisha kwamba nina ofisi katika kila kata ili niweze kuwafikia wananchi wangu katika kata zote kwani wakati napita kuomba kura ninawafuata na baada ya kufanikiwa kutimiza azma yangu ni wakati wa kuendelea kuwafuata na si wao kunifuata` alisema.
Kada huyo amesema sera yake kubwa itakuwa ni kumshirikisha kila mwananchi wa Kinondoni katika shughuli za kuleta maendeleo ili kila mtu aweze kutoa maoni, mawazo na mchango wa hali na mali katika kuleta maendeleo ya ukweli. Amesema hata mwananchi ambaye atakuwa hana uwezo, atabeba tofali kutoka upande mmoja hadi sehemu husika.
`nimeamua kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge kwa jimbo la hili ili niweze kuleta mageuzi makubwa sana katika jimbo la Kinondoni…naomba mfahamu kwamba kila mwananchi amebarikiwa akili, vipaji uwezo na Mwenyezi Mungu lakini asiposhirikishwa hataweza kutoa mchango wake, hivyo mimi nitahakikisha kwamba kila mmoja kwa uwezo wake na nafasi yake anachangia katika kuleta maendeleo`, alifafanua.
Shy-Rose alibainisha mambo makubwa ambayo atayapigania kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi ni elimu, afya, ajira kwa vijana, kupiga vita utumiaji wa madawa ya kuleta kwa vijana, kupigania haki za wasanii, kusaidia wajane katika kujikwamua kiuchumi na kuleta msukumo mpya kabisa katika masuala ya mahusiano na jamii ambayo kwa mtazamo wake eneo hili linahitaji msukumo mpya.
Shy-Rose amesema kwamba kutokana na uzoefu wa kazi zake tangu akiwa mwandishi wa habari, mtangazaji na Meneja uhusiano katika sehemu alizofanyia kazi, anaamini amekuwa mwanafunzi mzuri katika kutambua matatizo yanayoikabili nchi nzima na hususan na jimbo la Kinondoni.
`kwa kuzingatia uzoefu wangu ndani ya jamii ya kitanzania na baada ya kufikiria ni jinsi gani nitaweza kutumia akili, elimu yangu, uwezo, busara na vipaji vingi nilivyojaliwa na Mwenyezi Mungu na nafasi yangu katika jamii, hatimaye nikafikia uamuzi wa kujitosa kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hii.
`nimejifanyia tathmini ya kutosha, nimejiuliza maswali mengi na kutaka ushauri kutoka kwa viongozi wa chama, familia yangu, marafiki, na wanachama wenzangu. Nimefarijika kwa namna ya pekee walivyonihamasisha kutoka pande zote na ndiyo sababu ya kupata ujasiri wa kujitokeza na kuomba kuteuliwa ili nitimize azma yangu` alisema Shy-Rose.
Shy-Rose amesema ana kila sifa ya kujitosa na kuchaguliwa katika nafasi hiyo kwani yeye amekulia kwenye chama tangu akiwa kwenye Umoja wa Vijana wa CCM sehemu ambayo ni tanuri la kupika vijana kushika nafasi za uongozi na hatimaye kuiingia kwenye chama na viungo vyake.
`Mkiangalia CV yangu mtaona kwamba nimekulia kwenye chama, sijapitia tu kwenye chama, nimetokea ndani ya UVCCM, nimezunguka na viongozi mbalimbali wa chama na serikali nchi nzima na nimejifunza masuala mengi sana ya kutumikia jamii, na jinsi sera na ilani ya chama changu inavyofanya kazi zake za kila siku katika kutumikia wananchi.`, aliongeza.
Shy-Rose amesema sababu ingine iliyompa ujasiri wa kujitokeza katika nafasi hiyo ni kutokana na kauli mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi akiwemo Rais Jakaya Kikwete, za kuwataka wanawake kujitokeza katika kuwania nafasi za uongozi ili Tanzania iweze kufikia hatua ya kuwa na wabunge asilimia 50 wakiwa ni wanawake.
` kwa makusudi kabisa nimeamua kujitokeza kujitosa kwenye jimbo nikiamini kwamba ninaweza…iwapo nitashinda nitakuwa ni mfano mzuri kwa vijana wenzangu ambao wanapenda siasa lakini wametawaliwa na uoga wa kuingia hasa kwenye majimbo…kwangu mimi nataka niwe mfano wa kuigwa na kuhamasisha wanawake hasa wanawake vijana kuingia kwenye majimbo. Iwapo nitashinda basi mwaka 2015 vijana wengi zaidi watajitokeza kuingia majimboni tofauti na hivi sasa mwamko wao ni mdogo`. Alisema Shy-Rose ambaye kwa hivi sasa ni Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano Benki ya NMB Tanzania.
`kwa kuzingatia yote haya, nina kila sababu ya kuamini kwamba nina sifa za kutosha za kuteuliwa katika nafasi ya ubunge kwa jimbo la Kinondoni hasa kwa sera ya chama chetu ya kutaka kuwezesha wanawake kuingia katika nafasi za kutoa maamuzi (decision making bodies). Naamini kwamba iwapo chama kitanipitisha na hatimaye kushinda katika uchaguzi mkuu nitaweza pasipo shaka kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo makubwa ya kutatua kero za wananchi katika jimbo hili.
No comments:
Post a Comment