Monday, August 23, 2010

Mndorwa aibuka mshindi gofu Lugalo


Na Mwandishi wetu

Eddy Mndorwa amefanikiwa kuibuka mshindi katika mashindano ya mchezo wa gofu yaliyofanyika juzi katika viwanja vya mchezo huo vya Lugalo jijini Dar es Salaam baada ya kupata pointi 38.

Mndorwa aliyekuwa akichuana vikali na Simon Sayore alifanikiwa kumpiku kwa tofauti ya pointi 4 baada ya mpinzani wake kujipatia pointi 34.Ushindi huo ulimpatia Mndorwa zawadi mbalimbali kutoka Zain ikiwemo seti ya vyombo vya ndani.

Akiongea baada ya kukabidhiwa zawadi Mndorwa alisema akuamini wala akutarajia kama angekuwa mshindi kwasababu mchezo ulikuwa mgumu na kwamba alipata upinzani mkali kutoka kwa wachezaji wengine lakina hatimaye akaibuka mshindi.

“Siamini kama nimeshinda kwani mchezo kwangu ulikuwa mgumu sana na mpinzani wangu alikuwa mkali kweli lakini nimetumia vyema mashimo namba tisa na kumi ambayo yamenipa ushindi,” alisema Mndorwa

Mndorwa ambaye ni mchezaji mkongwe alisema yeye kumshinda Sayore ni furaha kubwa sana, kwakuwa alikuwa akisikia kuwa Sayore ni mchezaji mkongwe na mwenye uwezo mkubwa katika uchezaji wa mchezo wa gofu.

Mbali na Mndorwa washindi wengine ni Ally Mufuruki, Simon Sayore,Hassan Nkya na Bradray Mitchell Washindi hawa pia walijipatia zawadi mbalimbali ikiwemo miavuli, vyombo vya nyumbani pamoja vyote kutoka Zain.

Michuano hiyo ambayo imekuwa ikifanyika kila mwisho wa wiki chini ya udhamini wa Kampuni ya simu za mkononi ya Zain itaendelea wiki ijayo katika viwanja hivyo kwa kuwashirikisha wachezaji wa rika mbalimbali kutoka ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment