Saturday, October 23, 2010
TWIGA STARS WAPEWA CHAO KABLA YA KUSAFIRI
WACHEZAJI wa timu ya soka ya Wanawake 'Twiga Stars' wamezidi kuneemeka baada ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwachangia jumla ya sh.milioni 8.9.
Kiasi hicho cha fedha kilitolewa na Naibu Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, Joel Bendera alipokuwa akiikabidhi timu hiyo bendera ya taifa.
Mbali ya fedha hiyo kutoka kwa Wabunge, pia Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL)imetoa hundi ya Sh.milioni 83,137,500 pamoja na vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh.milioni 14.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Bendera alisema Wabunge waliona kuna umuhimu wa kuichangia timu hiyo ambapo baadhi ya wambunge walitoa kila mtu kiasi cha Sh.30,000.
"Nimeagizwa na Spika wa Bunge, Samwel Sita ili nilete fedha hiyo kwa ajili ya wachezaji na viongozi, na si ya TFF, hivyo moja kwa moja nimekabidhi kwa wachezaji wenyewe, na viongozi wao watazigawa," alisema Bendera.
Alisema, pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu kwa wachezaji wa timu hiyo, kwa kuwatakia kila lakheri na akawataka warudi na ushindi.
Bendera aliwataka wachezaji hao wajitume ili waweze kufanya vizuri katika michuano hiyo ya kimataifa na kuiletea sifa Tanzania, na kwamba hataki kuona wanarudi wakiwa na visingizio vingi.
Alisema imekuwa kawaida kwa timu za Tanzania pale zinaposhindwa kuleta visinguizio vingi, hivyo safari hii ametaka visiwepo kwa kuwa kila kitu wachezaji wamefanyiwa ikiwa na motisha mbalimbali kutoka kwa wadhamini.
Aliongeza kuwa tatizo kubwa ambalo linawakabili wachezaji wa Tanzania ni saikolojia, hivyo endapo watafanikiwa kumaliza tatizo hilo wanaweza kufika mbali katika michuano hiyo..
Kwa upande wa Meneja Bidhaa wa Kampuni ya Serengeti, Nandi Mwiyombewa, alisema wametoa kiasi hicho cha Sh,milioni 83, kwa ajili ya posho za wachezaji pamoja na malazi.
Alisema, pia wametoa na vifaa vya michezo kwa timu hiyo, zikiwemo jezi na viatu, ambavyo thamani yake ni sh.milioni 14.
Naye Kocha Mkuu wa timu hiyo, Boniface Mkwasa amesema wanaimani kubwa kwamba watafanya vizuri katika michuano hiyo kutokana na maandalizi waliyoyafanya.
Timu hiyo inashiriki michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wanawake, na kesho wanatarajiwa kwenda nchini Botswana kwa ajili ya mechi ya kirafiki, na baada ya hapo wataelekea nchini Afrika Kusini kwenye michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment