Wednesday, October 6, 2010
VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VISIINGILIE UCHAGUZI MKUU (FEMACT)
MASHIRIKA yanayotetea usawa wa jinsia, Haki za Binadamu, Maendeleo ya Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi (FemAct) umetoa msimamo wa kutokubaliana na tamko lilitolewa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kile kilichodaiwa kuingilia shughuli za uchaguzi.
Wakizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutoa tamko hilo Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayojihusisha na masuala ya utawala bora ForDIA, Good Govence Convencer FemAct Bw. Bubelwa Kaiza alisema;
"Tunashangaa kuona Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likifanyakazi za polisi wakati askari polisi wapo na Inspekta Jenerali wao hali hii haieleweki na nikinyume cha kanuni za msingi za utawala bora."
Bw. Kaiza aliendelea kuhoji; "Inakuwaje askari polisi wanaendelea kulipwa mshahara wakati kazi zao zinafanywa na wanajeshi wa JWTZ?"
Alisema kuwa ujumbe unaotolewa na tamko la vyombo vya usalama kuwa vimejiandaa kikamilifu kuwa vimeajindaa kupambana na mtu, watu, kikundi chama au taasisi yoyote itakayochochea kuyakataa matokeo ya uchaguzi ni kitisho cha dhahiri, sio kwa vyama vya siasa wala wagombee pekee bali dhidi ya jitihada za kujenga na kuimarisha utawala bora.
Wanaharakati hao kupitia tamko hilo walimtaka Luteni Jenerali Abdulhaman Shimbo kutambua kuwa sio wanajeshi wala silaha zinazoweza kulazimisha wananchi, vyama vya siasa na wagombea wao wakubaliane na matokeo ya chaguzi, bali unakubalika pale unapofanyika kwa kuzingatia vigezo vya msingi vya uchaguzi.
"Vyombo vya ulinzi na usalama viache mara moja kuingilia mchakato wa uchaguzi kwa kuwa jambo hili linaweza kusababisha vitisho na vurugu dhidi ya wapiga kura na wananchi kwa ujumla.
Wiki iliyopita maofisa waandamizi wa JWTZ na Polisi walitoa tamko la kuwataka wananchi kuyakubali matokeo ya uchaguzi vinginevyo limejiandaa kukabiliana na watu waliopanga kuyapinga.
Hata hivyo alisema kuwa tamko la vyombo vya ulinzi na usalama lina agenda yake ya siri, si bure litakuwa ni jambo la kushangaza na kusikitisha sana iwapo watanzania watabaini kuwa vyombo vyao vya ulinzi na usalama vimeanza kutumiwa vibaya na wanasiasa na vyama vyao kwa manufaa ya kikundi na maslahi binafsi kwa watu wachache.
Wanaharakati hao wamewataka vyama vya siasa na viongozi wao waache mara moja kujitafutia ushindi kwa kutumia mlango wa nyuma na kukubali matokeo.
Alisema kuwa uongozi wa dola sharti upatikane kupitia mashindano ya wazi kusaka ridhaa ya wananchi kidemokrasia katika uchaguzi unaokubalika kuwa huru na haki, siyo kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kutisha wapiga kura ili kujihakikishia ushindi.
Vile vile Bw. Kaiza alisema kuwa wapiga kura waendelee kujibidisha kupata elimu ya mpiga kura ,kuhudhuria mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa na kusikiliza ahadi za wagombea wapembue na kuchambua kati ya pumba na mchele ili Agosti 31 wafanye uamuzi wa kihistoria.
No comments:
Post a Comment