Tuesday, November 9, 2010

KCB yagawa madawati 300 kwa shule 12 jijini Dar es salaam

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mwantumu Mahiza (kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa KCB Tanzania Dk Edmund Mndolwa wakisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo mara baada ya kukamilika kwa hafla ya kukabidhi madawati 300 yenye thamani ya milioni 18.2 kwa shule 12 ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya jamii inayoandaliwa na benki hiyo kila mwaka kwa lengo la kuisaidia jamii inayowazunguka.
Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mwantumu Mahiza amekabidhi madawati 300 yenye thamani ya milioni 18.2/- yaliyotolewa na benki ya KCB Tanzania kwa shule 12 nchini na kusema anaondoka akijua bado shule nyingi zinakabiliwa na changamoto hiyo.

Shule saba zilizopatiwa msaada huo kwa awamu ya kwanza ni shule za msingi Mwanambaya madawati (15), Makuburi (30), Ruvuma(15) na Ali Hassan Mwinyi(15), shule za sekondari Hekima(30) na Msangani (30) pamoja na shule ya chekechea na msingi ya Bibi Jane (15). Awamu ya pili itakuwa kwa mikoa ya Arusha, Mwanza, Morogoro na Zanzibar.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Naibu waziri huyo alisema upungufu wa madawati ni tatizo linazozikabili manispaa nyingi nchini na serikali kwa ujumla hivyo kuzitaka kuongeza juhudi katika kulimaliza tatizo hilo ambalo linawezekana hata kwa kuwahusisha wazazi wa wanafunzi.

Akifafanua alibainisha kwamba ikiwa KCB Tanzania imeweza kutengeneza madawati kumi kwa kiasi cha milioni 1.5 iweke manispaa zishindwe wakati zikiwa na rasilimali tofauti ikiwemo rasilimali watu, miradi na mali.

“Kwa hili lililofikiwa leo nazishauri manispaa kujifunza na kuiga mfano huu wa KCB Tanzania wakati wakitumia changamoto hoi kujiuliza kwa nini taasisi hoi ya kifedha imeweza nao wanashindwa jambo litakalozibadilisha kifikra na kuleta maendeleo kwa jamii,” alisema Mahiza.

Mbali na hayo akizungumzia umuhimu wa msaada huo alisema ni urithi mzuri kwani utaweza kutumiwa kwa vizazi na vizazi tofauti Kama wangetoa madaftari ambayo yangeweza kutumiwa na mtoto mmojawapo peke yake.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwaasa walimu kuitangaza benki hiyo kwa wazazi wa wanafunzi na jamii kwa ujumla pia kuyatunza madawati hayo ili kuwapa moya wahisani wengine kuendelea kuzichangia shule hizo. Ambapo kwa upande wa wanafunzi aliwataka kuyatumia kwa kujiletea maendeleo katika masomo yao.

Awali Mwenyekiti wa Bodi wa KCB Tanzania Dk Edmund Mndolwa alisema kuwa katika kuadhimisha wiki ya jamii wametoa msaada huo kwenye sekta ya elimu ikiwa ni kawaida yao na kwamba kwa mwaka jana waliichagua sekta ya mazingira na mwakani wamependekeza kuwekeza kwenye sekta ya afya.

Dk Mndolwa alisema wanaendesha shughuli zao kwa umakini na kwa kuzingatia wajibu wao wa kusaidia jamii inayowazunguka. Aidha mbali ya shughuli za kibenki wanatoa misaada mbalimbali ili kupunguza umaskini hususani kwenye sekta ya elimu, afya, mazingira na maafa mbalimbali.

Kwa sasa benki hiyo ndiyo kubwa zaidi Afrika Mashariki ikiwa na matawi 200 na rasilimali. Ina mashine za kutolea fedha (ATM) zaidi ya 400 na mtandao unaozifikia nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Sudan Kusini.

No comments:

Post a Comment