Monday, April 18, 2011

CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO TANZANIA (TASWA) TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



1:Kamati ya Kusimamia Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) inaendelea na maandalizi yake kuhusiana na mambo mbalimbali.

Tayari kamati hiyo yenye wajumbe 18 imeshafanya vikao vyake mara mbili chini ya Mwenyekiti Masoud Sanani na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo, Juliana Yassoda ambaye ni mshauri kwenye kamati hiyo.

Pamoja na mambo mengine kamati imedhamiria kuiboresha tuzo hiyo itakayofanyika Mei 6, mwaka huu kwa mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kuwapata wanamichezo hao.

Kamati ilikubaliana kuweka vigezo maalum kwa ajili ya kuwapata wanamichezo hao, ambavyo vitakuwa mwongozo mzuri kwa shughuli hiyo, jambo ambalo tayari limekamilika na vitatangazwa wakati wowote kuanzia sasa.

Tayari kamati inayo majina ya wanamichezo kutoka vyama mbalimbali vya michezo, ambayo ni matatu ya wanaume na matatu ya wanawake kwa michezo ambayo jinsia zote mbili zinacheza. Na ile ambayo inachezwa na jinsia moja tu basi majina matatu kamati inayo.

Hata hivyo kamati inasikitishwa na baadhi ya vyama ambavyo bado havijawasilisha majina ya wanamichezo wake licha ya kupewa barua kuhusiana na jambo hilo kwa muda mrefu.

Tunaviomba vyama hivyo vijitahidi kuwasilisha majina kabla ya Jumanne Aprili 19, 2011, ili yafanyiwe kazi kama ambavyo ya vyama vingine yameshafanyiwa.

Pia kamati inaviomba vyama ambavyo vimewasilisha majina yao, lakini havikauinisha sifa za wanamichezo wake navyo vifanye hivyo kama vilivyoelekezwa kwenye barua ambazo viliandikiwa.

Mpaka kufikia leo majina ambayo kamati inayo ni ya michezo ya riadha, wavu, netiboli, kuogelea, soka, tenisi, karate, kikapu, ngumi za kulipwa, ngumi za ridhaa, gofu, mpira wa mikono, kriketi na paralimpiki.

2: Udhamini wa MultiChoice Tanzania

Aprili 19, 2011 Kampuni ya MultiChoice Tanzania itafanya mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi zao Barabara ya Ali Hassan Mwinyi saa tano asubuhi kutangaza udhamini wake kwenye Tuzo za Wanamichezo Bora wa Mwaka 2010.

Wadhamini wengine wa tuzo hiyo mpaka sasa ni Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ambao ni wadhamini wakuu, Hoteli ya Movenpick na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

3: Kamati ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) iliyokutana Aprili 9, mwaka huu jijini Dar es Salaam ilijadili mambo mbalimbali ikiwemo kuimarisha vyanzo vya mapato kwa chama na kushiriki kwenye masuala ya kuchangia jamii.

Kutokana na hali hiyo Kamati ya Utendaji iliteua Kamati Maalum kwa ajili ya kuandaa michezo mbalimbali ambayo fedha zitakazopatikana kiasi zitatumika kwa masuala ya kijamii kadri itakavyokuwa imeonekana na nyingine zitabaki kuimarisha chama lengo likiwa ni kukifanya chama kijitegemee kimapato.

Walioteuliwa kuingia kwenye Kamati hiyo na vyombo vyao kwenye mabano ni Majuto Omary (The Citizens), ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Kamati na Katibu wa Kamati atakuwa George John ambaye ni Katibu Msaidizi wa TASWA.

Wajumbe wa Kamati ni Sultani Sikilo (Mhazini TASWA), Somoe Ng’itu (Nipashe), Frank Balile (DarLeo), Asha Kigundula (JamboLeo),Angela Msangi (TBC1), Onesmo Kapinga, Grace Hoka na Zena Chande (Wajumbe TASWA) na Mwani Nyangassa (The African).

Moja ya mechi ambazo kamati itashughulikia ni ile ya mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2010/2011 na wachezaji bora wa ligi hiyo wa msimu wa mwaka 2010/2011, ambayo TASWA kikao ilishauri ifanyike Juni mwaka huu.

4:

Kikao hicho pia kilikubaliana yaandaliwe mafunzo mbalimbali kwa wanachama wake, na kuipa jukumu sekretarieti ya TASWA kuratibu suala hilo ili zipatikane semina tatu hadi kufikia Julai mwaka huu.

Amir Mhando

Katibu Mkuu TASWA/Katibu Kamati ya Tuzo

17/04/2011

No comments:

Post a Comment