Monday, April 11, 2011

Rooney asikitika kuikosa Manchester City


MCHEZAJI Wayne Rooney amesema kuwa amesikitishwa kwa kukosa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester City, baada ya rufaa yake kutupiliwa mbali na kutakiwa kutumikia adhabu ya kutocheza mechi mbili.

Mshambuliaji huyo wa Manchester United alikubali shitaka lake la kutukana mbele ya kamera za televisheni baada ya kufunga mabao matatu kwenye mchezo dhidi ya West Ham siku ya Jumamosi.

Lakini alikata rufaa dhidi ya adhabu aliyopewa akisema imepita kiasi.

"Hii si sawa," imesema taarifa kutoka kwa Rooney, ambaye pia atakosa mchezo wa Jumamosi dhidi ya Fulham.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alitoa taarifa muda mfupi baada ya adhabu hiyo kuthibitishwa na kuongeza: "Nimesikitishwa kukosa mechi mbili, moja ya Kombe la FA kwenye uwanja wa Wembley. "Mimi si mchezaji wa kwanza kutukana mbele ya televisheni, na sitokuwa wa mwisho.

"Tofauti na wengine walioonekana wakitukana kwenye kamera, mimi niliomba radhi mara moja. Lakini mimi ndio mtu pekee niliyeadhibiwa kwa kutukana. Hii si sawa,"alisema.

"Vyovyote vile, nimekubali adhabu hiyo. Kilichotokea kimetokea, na tutaendelea na shughuli zetu. Hiyo ndio dhamira yangu."aliongeza.

Manchester United pia imetoa taarifa ikisema "imesikitishwa sana".

Taarifa hiyo ilieleza kuwa "Klabu iliwasilisha kesi yake kutaka adhabu kupunguzwa, ambayo hata hivyo haikufanikiwa.

"Wayne Rooney aliomba radhi mara moja baada ya mchezo, na sasa klabu itaendelea na shughuli zake katika msimu huu ambao bila shaka utakuwa wa kusisimua."

Licha ya kutumikia adhabu hiyo, Rooney ataweza kucheza mechi ya marudiano ya robo fainali ya klabu bingwa Ulaya dhidi ya Chelsea kwenye uwanja wa Old Trafford siku ya Jumanne.

No comments:

Post a Comment