Friday, June 17, 2011

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango awasilisha bajeti ya (SMZ)


Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo,Omar Yussuf Mzee amewasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 akiahidi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora atatangaza viwango vipya vya mishahara hapo baadaye. “Kuhusu suala la mishahara ya Watumishi wa Umma,Serikali tayari imefanya mapitio na kuandaa mapendekezo mapya ya mishahara ambayo itaanza kutumika mwaka wa Fedha 2011/2012” Alisema Waziri huyo wa Fedha. Alisema mapendekezo hayo ya mishahara mipya yamezingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu aliyonayo mtumishi, uzoefu na muda aliofanyakazi. “Miundo ya Utumishi imewapanga watumishi na nyongeza zao za mishahara kwa kuzingatia muda wa uajiri na kiwango cha elimu…mbali ya hatua zinazochukuliwa,Serikali itakuwa ikiongeza maslahi ya watumishi wa umma kila mwaka pale hali ya uchumi na mapato ya Serikali itakapokuwa nzuri” Aliongeza Waziri Mzee. Waziri huyo alisema bajeti hiyo inalenga zaidi katika kuimarisha na kuleta maendeleo ya kiuchumi pamoja na maslahi ya wafanyakazi na wananchi kwa ujumla. Akizungumzia kuhusu uchumi, Waziri huyo alisema kwa mwaka 2010 uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua ingawa kwa kasi ndogo ikilinganishwa na mwaka 2009. Alisema kwa bei za huduma mwaka 2001,pato halisi la Taifa la Zanzibar limekuwa kwa asilimia 6.5 na kufikia shilingi za Kitanzania bilioni 385.4 mwaka 2010 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.7 mwaka 2009 ambapo pato la Taifa lilikuwa kwa shilingi bilioni 361.9. Waziri huyo alisema kuwa kasi ya ukuahi imeonekana kuwa chini ya makadirio yaliyotarajiwa ya kufikia ukuaji wa asilimia 7.0. “ Hali hii inatokana na kushuka kwa kasi ya ukuaji wa sekta ndogo za umeme,viwanda,ujenzi na utalii” Alisema Waziri Mzee . Aidha, ukuaji wa sekta ya huduma umeonekana kupungua kutoka asilimia 8.8 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 8.7 mwaka 2010. Waziri Mzee ameliambia Baraza kwamba hali hiyo imetokana na kupungua kwa shughuli mbalimbali za huduma zikiwemo hoteli na mikahawa ambazo zilikuwa kwa asilimia 3.0 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 5.0 mwaka 2009. Katika hatua nyengine, Waziri huyo amewaeleza Wajumbe kwamba SMZ inaendelea na juhudi za maandaalizi ya uchimbaji wa mafuta na gesi kwa upande wa Zanzibar. Kuhusu deni la Taifa, Waziri Mzee alisema hadi kufikia mwezi Machi mwaka wa Fedha 2010/2011 malipo ya marejesho ya mikopo ya ndani yalifikia shilingi 1.76 bilioni sawa na asilimia 29.3 ya makadirio katika kipindi hicho. Kuhusu pato la Taifa, Waziri huyo alisema kwa mwaka 2011/2012 pato la Taifa linatarajiwa kukua kwa kasi zaidi kutoka ukuaji wa asilimia 6.5 hadi kufikia asilimia 7.9 Alisema kutokana na athari za mabadiliko ya bei z chakula na mafuta ya nishati duania, kasi ya mfumko wa bei inatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 6.1 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7. Akizungumzia mapato ya Serikali, Waziri huyo alisema katika mwaka wa fedha 2011/2012 inatarajia kukusanya shilingi 613.08 bilioni ikilinganishwa na shilingi 444.64 bilioni mwaka 2010/2011 ikiwa ni ziada ya shilingi bilioni 168.44 bilioni sawa na asilimia 38. Alisema hali hiyo inatokana na kuimarika kwa makusanyo ya ndani na kuongezeka kwa misaada ya Washirika wa Maendeleo. Aidha, alisema jumla ya shilingi 221.24 bilioni zinatarajiwa kukusanywa kutokana na vyanzo vya kodi na shilingi 11.02 bilioni kutokana na vyanzo visivyokuwa vya kodi. Alisema mapato ya ndani yanatarajiwa kuongezeka kwa shilingi 49.55 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 28.86 ambapo makusanyo ya ndani yanatarajiwa kuwa sawa na asilimia 20.2 ya pato la Taifa. Aidha, alisema ongezeko kubwa la mapato ya TRA linategemea kutekelezwa kwa makubaliano ya kukusanya kodi ya mapato kwa wafanyakazi wa SMT waliopo Zanzibar kulipwa Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetenga jumla ya shilingi 613,076 bilioni kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ambapo kazi za Maendeleo zimetengwa shilingi 378,901 bilioni huku kazi za kawaida ni shilingi 234,175 bilioni.

No comments:

Post a Comment