Thursday, August 4, 2011

MSAJILI HANA UWEZO KUFUTA CHAMA CHA SIASA AMBACHO WABUNGE WAKE WANAFANYA FUJO


JOSEPH ISHENGOMANA MPOKI NGOLOKE

MAELEZO

Msajili wa vyama vya siasa amesema kuwa ofisi yake haina nguvu kisheria kifuta chama chochote cha siasa kutokana na wabunge wake kukosa heshima bungeni.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo jinini Dar es Salaam Bwana John Tendwa amesema Bunge ni Mhimili mwingine wa serikali baada ya Mahakama na Utawala, na kuna kanuni lililojiwekea za kuwaongoza kufanyakazi.

Hivi karibuni kumekuwepo na vitendo vya vurugu bungeni, kuwasha vipaza sauti ovyo na kupiga kelele bila kuruhusiwa na Spika au Mwenyekiti wa Bunge. Hali hii imesababisha wabunge kadhaa kutolewa nje ya bunge kutokana na kukiuka kanuni.

“Wabunge wakiwa ndani ya bunge sio wangu, sina madaraka nao, lakini wakiwa nje ya kuta za bunge ni wangu. Ndani ya Bunge mikono na midomo yangu imefungwa kabisa, lakini kwa mtazamo wa wananchi wanajua kuwa mimi ninamamlaka ya kuwawajibisha kutokana na utovu wa nidhamu wanouonyesha bungeni, lakini sio,” amesema

“Mimi nimechukia sana kuona vitendo hivi kwasababu natupiwa lawama na watu kuwa wanaofanya vurugu bungeni ni watu wanaotoka katika vyama vyangu. Ninafurahi kwakuwa vyama vyangu nilivyovisajili viko ndani ya bunge, lakini sifurahishwi na utovu wa nidhamu wanaofanya”

Kwa mujibu wa Msajili wa vyama vya Siasa, baadhi ya wabunge vitendo wanavyofanya ndani ya Bunge kila anayesikia au kushuhdia vitendo hivyo, lazima asikitike.

“Taratibu na mamlaka ya kudhibiti utovu huo wa nidhamu uko ndani ya Bunge. Bunge ni taasisi inayojitegemea haiingiliwi na upande wowote (Mahakama na Utawala).

Baadaye mwezi huu, Msajili wa Vyama vya Siasa atakutana na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa katika baraza la vyama na kuwaelezea masikitiko yake.

“Tutakuwa katika baraza la vyama kabla ya bunge lijalo. Tutazungumzia hali hii na kutoa jibu,” amesema

No comments:

Post a Comment