Friday, August 19, 2011

NI SIMBA,SIMBA, SIMBAAAA KILA KONA


Mashabiki wa Simba wakishangilia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya watani wao wa jadi yanga katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii, kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji wa Simba wakishangilia ushindi wa bao la pili dhidi ya watani wao wa jadi Yanga.

SIMBA, Simba ndio ulikuwa wimbo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada vijana hao wa mtaa wa Msimbazi kulipinza kisasi kwa ukifunga Yanga mabao 2-0 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.

Simba waliofungwa kwenye Kombe la Kagame na Ngao ya Jamii mwaka jana vijana hao wa Mganda Moses Basena walizinduka na kupata mabao ya mapema kupitia kiungo Haruna Moshi 'Boban' dakika 15 na penalti ya Felix Sunzu dakika 38.

Simba iliyoanza kwa kasi mchezo huo ilifanikiwa kupata bao la kuongoza kupitia kwa Moshi 'Boban' aliyemalizia vizuri krosi ya kutoka upande wa kushoto iliyopigwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Sunzu aliyekuwa na ushirikiano mkubwa na Emmanuel Okwi.

Mshambuliaji Sunzu alifungia Simba bao la pili kwa mkwaju wa penalti baada ya Nadir Haroub kumchezea vibaya Moshi 'Boban', kwenye eneo la hatari dakika 35. Sunzu alilazimika kuonyesha ueledi wake pale alipotakiwa kurudia penalti hiyo baada ya mwamuzi Israel Mjuni kusema Kado alitokea kabla ya kupigwa kwa penalti ya kwanza pamoja na kuwa alikuwa amefunga.

Kocha Moses Basena aliyeonekana kujifunza kwa makosa alitumia mfumo wa 4:2:3:1 na kutoa nafasi kubwa kwa Okwi, Haruna na Sunzu kutawala sehemu kubwa ya kiungo tofauti na ilivyokuwa kwenye fainali ya Kombe la Kagame.

Okwi alifanya atakalo mbele ya mabeki wa Yanga walionekana kuwa kama watu waliozidiwa na mazoezi na kukosa unyumbulifu mchezoni, huku safu ya ulinzi wa Simba chini ya mkongwe Victor Costa aliweza kuwapoteza mchezoni kabisa mshambuliaji Keneth Asamoah na Jerry Tegete.

Kiungo Haruna Niyonzima alijitahidi kuonyesha uwezo mkubwa wa kutawala mpira na kujaribu kutafuta goli kwenye mechi yake ya kwanza ya watani wa jadi, lakini alikosa msahada kutoka kwa wenzake.

Simba ilianza mashambulizi kwa kasi na dakika kwanza Okwi alikosa bao baada ya shuti lake kumgonga Haroub na kupaa juu ya goli.

Okwi alipoteza nafasi nyingine dakika 8 baada ya kuwalamba chenga mabeki wa Yanga, lakini aliugonga mpira mbele zaidi na kipa Shaaban Kado akauwahi.

Beki wa Yanga, Chacha Marwa, nahodha Shadrack Nsajigwa alipewa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Okwi. Naye Juma Nyoso wa Simba alipewa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Asamoah.

Haruna Niyonzima alipiga shuti la umbali wa mita 25 baada ya kumchungulia Juma Kaseja kwa bahati mpira huo ulipaa juu ya goli.

Kipindi cha pili Yanga iliamka baada ya kuingia Hamisi Kiiza na Rashid Gumbo lakini walishindwa kuipenya ngome ya Simba.

Yanga waliendeleza sera yao ya kugomea jezi za wadhamini wa ligi Vodacom zenye nembo nyekundu kwa kuvaaa jezi za mdhamini wao TBL tofauti na Simba wenyewe walivaa zile walizopewa na Vodacom

Vikosi Yanga; Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Chacha Marwa, Juma Seif, Godfey Taita, Haruna Niyonzima, Keneth Asamoah/ Gumbo, Jerry Tegete, Kigi Makasi/ Kiiza.

Simba: Juma Kaseja, Said Nasoro, Amir Maftah, Juma Nyoso, Victor Costa, Partick Mafisango, Salum Machaku/ Kiemba, Jerry Santo, Felix Sunzu, Haruna Moshi/ Gervais Kago, Emmanuel Okwi/ Kapombe.


http://richard-mwaikenda.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment