Monday, August 29, 2011

WAKALI WA JAHAZI WATIMKIA KUNDI JIPYA LA T MOTO MORDEN TAARAB ‘REAL MADRID’

Joha Kassim, akiimba wakati wa mazoezi na kundi lake jipya la T-Moto Morden Taarb.

Mrisho Rajab, mshiriki wa BSS 2011, akighani rap zake zitakazotumika katika baadhi ya nyimbo hizo mpya.
Hassan Ali, aliyetoka kundi la Fife Star, akiwa katika mazoezi hayo.

*Mtoto wa Salmini afanya kufuru, abomoa makundi ya jahazi na five star
*Asema kundi hilo ni kama ‘Real Madrid’
*Kutambulishwa na Aliyeniumba Hajanikosea
MTOTO wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amin Salmin ‘Mourinho’, amenzisha kundi jipya la muziki wa Taarab linalojulikana kwa jina la T Moto Morden Taarab ‘Real Madrid’ linaloundwa na wasanii mahiri waliopata kutamba katika makundi ya Jahazi Morden Taarab, Five Star na mengineyo.

Akizungumza na Sufianimafoto, Amin alisema kuwa ameamua kuleta mabadiliko na ushindani katika muziki wa taarab kutokana na muziki huo kutokuwa na makundi yenye ushindani wa kisanii zaidi ya majungu na kufanya baadhi ya makundi yakivunjika kwa kushindwa kutoa upinzani na kubuni vitu vipya vinavyoweza kusaidia kulibakiza kundi katika jukwaa la muziki huo.

Aidha alisema kuwa ni siku nyingi alikuwa na ndoto ya kumiliki kundi la muziki wa Taarab, kutokana na kuvutiwa zaidi na muziki huo, lakini amekuwa akisikitishwa na baadhi ya wanamuziki wa taarab wanaopotea na vipaji vyao ama kushindwa kuwa na maisha mazuri hali ya kuwa wanakuwa wamefanya kazi kubwa ambayo hutokea kupendwa na mashabiki na kuuzika.

Amini anayejiita Mourihno kutokana na ‘kusajili’ wanamuziki nyota kutoka katika makundi makubwa ya muziki huo amesema kuwa wanamuziki aliowapata kuunda kundi hilo, anatarajia kuwa kundi hilo litafanya mambo mazuri na makubwa yatakayowashitua mashabiki wa muziki huo kwa kipindi kifupi kutokana na umahiri wa wanamuziki hao wenye hari zaidi na morari ya kufanya kazi kwa mageuzi na maslahi.

“Kutokana na kuuelea vyema muziki huu, kundi letu tumeamua kutumia aina ya kipee kati ya makundi yote yanayopiga muziki huu kwa kutumia jumla ya magitaa matatu ili kuweza kuleta radha na vionjo tofauti vya muziki huu, tofauti na makundi mengine ya taarab ambayo hutumia magitaa mawili tu” alisema Amini.

Aliwataja wanamuziki wanaounda kundi hilo jipya kwa upande wa waimbaji kuwa wanaongozwa na mwanamuziki mkongwe, Mwanahawa Ali, Mosi Suleiman aliyetoka kundi la Dar Morden Taarab, Joha Kassim, kutoka kundi la Five Star, Hasina Kassim, kutoka kundi la New Zanzibar Morden Taarab, Hassan Ali kutoka kundi la Five Star na Mrisho Rajab mshiriki wa BSS 2011.

Kwa upande wa wapiga vyombo wanaongozwa na mpiga Solo, Jumanne Ulaya ‘Mkono wa Biashara’ aliyetoka kundi la Jahazi Morden Taarab, Wapiga kinanda ni pamoja na Amour Saleh Zungu, aliyewahi kupita katika bendi za Twanga Pepeta, TOT na nyinginezo, Moshi Mtambo, kutoka kundi la New Zanzibar Morden Taarb na Omary Kisila kutoka, wengine ni pamoja na mpiga gitaa la rythim, Fadhili Ali Mnara, aliyekuwa katika muziki wa dansi katika baadhi ya Hoteli na mpiga Gitaa la Besi, Rajab Kondo kutoka kundi la New Zanzibar na Mussa Mipango, nayefanya kazi kwa mkataba kutoka kundi la TOT.

Aidha Amini alisema kuwa Kundi hilo hivi sasa bado linaendelea kujifua kuandaa vitu vipya ikiwa ni pamoja na nyimbo sita ambapo nne kati ya hizo zitaitambulisha albam yao ya kwanza itakayokwenda kwa jina la Aliyeniumba Hajanikosea, uliotunga na kuimbwa na Bi Mwanahawa Ali.

Nyimbo nyingine ni, Mtoto wa Bongo, inayoimbwa na Hassan Ali, Unavyojizani Mbona Hufanani, inayoimbwa na Joha Kassim, Mchimba Kaburi Sasa Zamu yake Imefika, inayoimbwa na Mrisho wa BSS, Mwenye Kustili Mungu na kumbe Wewe ni Shoti zote zikiimbwa na Mosi Suleiman, ambapo moja kati ya hizo itakuwa katia albam ya.

Kundi hilo limeingia Studio leo Agosti 29 kwa ajili ya kuanza kurekodi nyimba zake mpya ambazo kwa pamoja zitaanza kusikika hivi karibuni.

Naye kiongozi wa kundi hilo, Jumanne Ulaya ‘Mkono wa Biashara’, aliwataka wapenzi wa miondoko hiyo ya Taarab, kukaa mkao wa kula wakisubiri vitu vipya kutoka kwa kundi hilo vyenye utofauti mkubwa na ambavyo vitakuwa na radha ya kutochosha kusikiliza.

“Nawaahidi tu wapenzi wa muziki wa Taarab wakae mkao wa kula wasubiri kusikia kilichotuingiza kambini na nyimbo ambazo kwa kweli hazichoshi kusikiliza, kwani tumetua kundi hili kikazi zaidi na majungu” alisema Jumanne

No comments:

Post a Comment