(Na Esther Muze na Bebi Kapenya – MAELEZO)
Serikali ya Tanzania imepokea msaada wa shilingi bilioni 133 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa ajili ya kusaidia miradi kuendeleza sekta ya kilimo na elimu nchini.
Msaada huo ulisainiwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa fedha Mustafa Mkulo kwa niaba ya Tanzania na Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Tonia Kandiero.
Akiongea mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri wa Fedha alisema kuwa, fedha hizo zitasidia katika kuboresha sekta ya kilimo ikiwemo miundombinu ya masoko .
Aliongeza kuwa, sehemu nyingine ya fedha hizo itasaidia kutoa mafunzo kwa vijana wenye mahitaji maalum ambao walioacha masomo kabla ya kumaliza elimu yao kwa sababu mbalimbali.
Mkulo aliahidi kuwa Serikali ya Tanzania itahakisha kuwa msaada huo unatumika katika maeneo waliyokubaliana ili kuleta maendeleo kwa kwa wananchi na kupunguzia umaskini.
Naye Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Tonia alisema kuwa, msaada uliotolewa na Benki hiyo utasaidia Tanzania kiuchumi katika harakatio zake za kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
Aliongeza kuwa msaada huo utawasaidia vijana kupata ujuzi katika visiwa vya Zanzibar ambao watasaidia kuongeza nguvukazi katika soko la ajira kwa ajili ya kuleta maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
Aidha alisema kuwa Benki hiyo itaendelea kuisaidia Tanzania ili kukuza maendeleo yake ya kiuchumi na kijamii.
Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa miaka mitatu iliyopita imekuwa ikitoa misaada ya kifedha kwa lengo la kuisaidia Tanzania kiuchumi.
No comments:
Post a Comment