Monday, September 5, 2011

BALOZI WA MAREKANI NCHINI TANZANIA KUFUNGUA MAFUNZO YA MCHEZO WA MPIRA WA KIKAPU kesho


Moshi Stewart (MAELEZO)

DAR-ES-SALAAM

Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani nchini pamoja na wadau wao wengine kama Coca-Cola kupitia kinywaji cha Sprite na Family Healthy International (FHI) wameandaa ziara ya kimichezo ya mafunzo ya mchezo wa kikapu (Basketball) yatakayotolewa na wachezaji wa zamani wa ligi kubwa ya mpira wa kikapu duniani ya NBA na WNBA

Akiwaeleza waandishi wa habari Makamu wa Raisi wa Shirikisho la Mpira wa kikapu Tanzania (TBF) Bw. Phares Magesa aliwataja wachezaji wanaotarajiwa kuwasili leo jioni ni Tamika Raymond (WNBA), Becky Bonner (WNBA) na Dee Brown (NBA) aliyechezea Dallas Mavericks na kwamba ni wachezaji nyota katika ligi za Marekani

Akiongezea Bw. Phares amesema msafara huo wa wachezaji hao ndio watakaotoa mafunzo katika kliniki iliyoandaliwa hapa nchini watawasili leo tarehe 5/9/2011 saa 12:50 jioni na wataanza kutoa mafunzo kesho (leo) tarehe6/9/2011 hadi tarehe8/9/2011 na wataondoka nchini tarehe9/9/2011

Mafunzo hayo yatafunguliwa na Balozi wa Marekani nchini Mheshimiwa Alfonso E. Lenhardt saa 2:30 asubuhi katika viwanja vya Don Bosco, Upanga. Aliongeza kuwa kliniki ya mwaka huu ni ya tofauti kidogo na zilizofanyika miaka ya nyuma kwani itawakutanisha vijana zaidi ya100 walio na umri chini ya miaka16 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.

Akiitaja mikoa hiyo ni Dar-es-saalam, Kagera, Mara, Tabora, Mtwara, Ruvuma, Singida, Visiwa vya Zanzibar, Shinyanga, Kigoma, Iringa, Rukwa, Lindi na Kilimanjaro ambapo kila mkoa utawakilishwa na vijana 3 waliochini ya umri wa miaka 16 wa kike na kiume na Mwalimu 1 wa kikapu.

Bw. Magesa ameongeza mbali na mafunzo hayo kwa vijana pia watatembelea na kuongea na wanafunzi wa shule ya Msingi Mazoezi ya Chang’ombe na sekondari za Makongo na Jitegemee pia watapata nafasi ya kutembelea maeneo mengine ya Jiji la Dar-es-saalam na kujionea baadhi ya vivutio na utamaduni wetu wa kijiji cha Makumbusho na maduka ya kuuza vinyago maeneo ya Mwenge

Akimalizia Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) Ndugu Magesa kupitia fursa hiyo amewaomba wadau na Watanzania kwa ujumla wajitokeze kwa wingi katika viwanja vya Don Bosco, Upanga siku ya ufunguzi na siku zote za mafunzo ili kushuhudia .

No comments:

Post a Comment