Thursday, September 22, 2011

Mbunge Bi Zarina Madabida Awacharukia Wanaharakati


Mbunge wa Viti Maalum Bi.Zarina Madabida akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake Mikocherni Dar es Salaam jana .Pamoja na mambo mengine pia aliwataka wana harakati kumwekea wakili Mkuu wa wilaya ya Igunga Bi.Fatuma Kimario katika kesi aliyoifungua wilayani humo kupinga udhalilishaji aliofanyiwa na wanachama wa Chadema hivi Karibuni.


MBUNGE wa Viti Maalum (CCM),Bi. Zarina Madabida amedai kushangazwa na ukimya uliofanywa na wanasheria na wanaharakati wanawake kutojitokeza kumtetea Mkuu wa Wilaya ya Igunga Bi. Fatuma Kimario ambaye alidhalilishwa na wafuasi wa CHADEMA kama wanavyofanya kwa wanawake wengine ambao wamefanyiwa vitendo hivyo.

"Nashindwa kuelewa TAWLA,TGNP,TAMWA na wanaharakati wengine wanaotetea haki za wanawake wamekaa kimya bila kutolea maamuzi suala tuwaeleweje. Hii inanipa mashaka makubwa,"alisema.

Bi. Madabida alisema kuwa wanaharakati hao siku zote wapo mstari wa mbele kutetea wanawake na watoto ikiwemo jamii, lakini anashangazwa na ukimya kuhusu utetezi wa Bi. Kimario.

Alisema mbona wanawake wakiwa wananyanyaswa wanakuwa mstari wa mbele kutetea lakini iweje leo hii aliyefanyiwa hivi ni mwanamke tena kiongozi lakini wamekaa kimya tuwaeleweje?.

"Hawa tuwaeleweje ni wanawaharakati au wao wanavyama vingine vya siasa, utetezi wao huko wapi inanipa mashaka,"alisisitiza

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Chama Cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA)Bi.Analelia Nkya alipoulizwa juu ya kimya walichonacho kuhusu kudhalilishwa na Bi. Kimario alishindwa kutoa tamko kuhusu udhalilishaji huo kwa madai kuwa wao wanashughulikia masuala ya jamii na wala siyo ya mtu mmoja.

"Sisi tumekuwa tukizungumzia masuala ya jamii na sio suala la mtu mmoja sasa wewe kama mwandishi ukiniuliza tumekaa kimya kuhusu kudhalilishwa kwa mwamamke mwenzetu nakushangaa sana,"alisema Bi. Nkya.

Hivi karibuni wafuasi wa CHADEMA walimkamata Mkuu huyo wa Wilaya na Kumdhalilisha kwa madai kuwa alikuwa anapanga njama za kuupatia ushindi CCM katika uchaguzi mdogo unaoendelea jimboni humo,wakati alipokuwa akizungumza na watendaji wa wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment