KAMATI Maalumu ya Kudhibiti na Kuboresha mapato ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imependekeza zitumike tiketi za eletroniki katika mechi mbalimbali ,badala za karatasi na kuweka ving’amuzi milangoni, ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato hayo.
Pia, imetaka tiketi hizo ziuzwe na mawakala maalumu watakaopatikana kwa zabuni ya wazi, ili kila mwenye sifa ajitokeze, ambapo shirikisho hilo lisijihusidhe na kuuza tiketi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Rais wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga, amesema baada ya mchakato wa muda mrefu na uchunguzi wa suala hilo, wamefanikiwa kupata ufumbuzi, hivyo imebaki utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na kamati.
Tenga amesema ili kuondokana na matatizo ya mapato, kamati imependekeza zianze kutumika tiketi za eletroniki kwani ana imani tiketi bandia, hazitakuwepo tena.
Amesema tiketi hizo zitasaidia kufanya uhakiki wa mapato kwa vile yatakuwa yakifahamika mara moja, kadri zitakavyokuwa zikiuzwa katika mechi mbalimbali.
Mwenyekiti huyo wa kamati amesema ripoti hiyo, pia imebainisha upungufu uliopo katika miundombinu ya viwanja kwamba haifanani na dunia ya leo, hivyo Idara ya Ufundi ya shirikisho hilo itazungumza na wamiliki wa viwanja ambao ni serikali, CCM na baadhi ya manispaa ili kuboresha viwanja hivyo.
Amesema ukiangalia hivi sasa watu wengi wanaogopa kwenda uwanjani kutokana na ushabiki uliopo unaofanya wengine kukosa amani, hivyo wataboresha usimamizi wa nidhamu ya watazamaji, ili uvutie kwa kila mtu kwenda ikiwezekana na familia zao.
No comments:
Post a Comment