Thursday, November 3, 2011

Exim yatoa bil 13 kwa wanawake wajasiriamali


Na Mwandishi Wetu

BENKI ya Exim Tanzania imetoa mikopo ya shilingi bilioni 13 kupitia program yake ya Uwezeshaji wa Kifedha kwa Wanawake Wajasiriamali (WEF) katika kipindi cha miaka 4.

Afisa wa Programu hiyo wa Benki ya Exim, Bi. Neema Langa aliyasema hivi karibuni katika maonyesho ya wanawake wajasiriamali (MOWE) yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa kupitia mpango huo wa uwezeshaji kwa wanawake wajasirimali benki yao imeweza kuwasaidia wanawake ikiwa na lengo la kuinua vipato vya wanawake hao katika ngazi ya familia kwani wanawake ni mhimili muhimu katika taifa zima.

“Tangu mpango huu wa WEF ulipoanza mwaka 2007 mpaka sasa, tumeshawafikia wanawake wajasiriamali wadogo, wakati na wakubwa 300 tukiwapatia elimu na ushauri wa jinsi ya kuanzisha na kuendesha biashara mbalimbali katika ujasiriamali, mikopo yenye riba nafuu na jinsi ya kutumia fursa mbalimbali za kibiashara zinazojitokeza katika sekta hii ya ujasiriamali”, alisema Neema.

Aliongeza kuwa wamekuwa pia wakitoa udhamini katika shughuli tofauti za kimaendeleo hasa wakiwalenga wanawake ambao ni chachu ya maendeleo katika jamii.

Kwa upande wake, Meneja Wanawake wa mpango huo, Bi. Felister Simba, alisema kuwa kama kauli mbiu ya maonyesho hayo inavyosema ‘Miaka 50 wanawake wajasiriamali twaweza tutumie fursa’ kwamba ni wakati muafaka kwa wanawake wote nchini kutumia fursa zote zinazojitokeza na kuwekeza kupitia ujasiriamali ili kujikwamua kiuchumi.

“Kama Exim Bank Tanzania tumekuwa katika mstari wa mbele kupitia mpango wetu wa WEF tumeweza kuwawezesha wanawake wajasiriamali kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza katika biashara pamoja na kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kupitia WEF tumewafungulia akaunti maalum ya wanawake wajasiriamali ya Tumaini Akaunti yenye vigezo rahisi katika ufunguaji wake”, alisema Bi. Felister.

Aliongeza kuwa lengo kuu la kushiriki katika maonyesho hayo ni kuwahamasisha wanawake kujiunga katika mpango huo wa WEF unaoendeshwa na benki hiyo na kuwahamasisha wajiunge katika sekta ya ujasiriamali ili wajikwamue kiuchumi.

Benki ya Exim Tanzania ni miongoni mwa benki za kizalendo nchini zinazopiga hatua kubwa katika sekta ya kibenki ikiwa na matawi 21 nchini na mengine 3 katika nchi za Comoro na Djibouti huku ikiwa na mkakati wa kufungua huduma zake nchini Zambia.

No comments:

Post a Comment