Monday, November 7, 2011

MABADILIKO YA TAREHE YA MWISHO YA UCHUKUAJI FOMU KWA WAGOMBEA KWENYE CHAGUZI ZA MASHIRIKISHO YA SANAA NCHINI



Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) liko kwenye mchakato wa kuwaunganisha wasanii wote nchini kupitia vyama na mashirikisho kwa lengo la kuunda umoja wa wasanii wenye nguvu utakaopambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Mchakato huo ulifikia katika mafanikio ya kufanyika kwa chaguzi za mashirikisho manne ya Sanaa nchini ambayo ni Muziki, Sanaa za Ufundi, Maonyesho na Filamu mwaka jana ambapo viongozi wa muda walipatikana na kupewa majukumu ya kuandaa mipango mikakati ya mashirikisho, kanuni na baadaye kukabidhi majukumu kwa viongozi wa kikatiba.

Hata hivyo, viongozi hao wa muda kwa sasa wanamalizia muda wao wa mwaka mmoja hivyo, kulifanya Baraza kuanza zoezi la kuratibu na kusimamia chaguzi za viongozi wa kikatiba watakaodumu Madarakani kwa miaka mitatu.

Kwa mujibu wa Sekretariati za Mashirikisho hayo, Fomu za wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi zimeshaanza kutolewa ambapo zoezi la uchukuaji na urejeshaji lilipaswa kuwa limefikia tamati Tarehe 30/10/2011.

Lakini kutokana na maombi maalumu ya Sekretariati hizo BASATA linapenda kuwafahamisha Wasanii wote nchini kuwa, tarehe ya mwisho ya zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu za wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye chaguzi za Mashirikisho imesogezwa mbele kutoka Tarehe iliyotajwa hapo Juu yaani 30/10/2011 hadi Siku ya Jumanne Tarehe 8/11/2011 Saa 10.30 Jioni.

Nia na lengo la kusogeza muda huo ni kuwapa fursa Wanachama wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa Mashirikisho waendelee kuchukua na kurudisha fomu kwa Sekretariati zao za Mashirikisho.

Aidha, BASATA linawafahamisha wadau kuwa, Tarehe 9/11/2011 na 10/11/2011 upitiaji wa fomu za wagombea utafanyika na Tarehe za 22 na 23 za Mwezi huohuo wa Novemba zimetengwa maalum kwa wadau kutoa maoni kuhusu majina mbalimbali ya wagombea watakaokuwa wamejitokeza miongoni mwa wasanii/wanachama.

BASATA linatoa wito kwa Wasanii/Wanachama kujipanga katika vyama vyao na kuhakikisha viko hai kwa ajili ya kushiriki chaguzi za mashirikisho zinazotarajiwa kufanyika Mwezi Desemba mwaka huu.

Moja ya njia ambayo itawaunganisha wasanii katika kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili ni kwa kuimarisha vyama na mashirikisho haya. Ni vema Wasanii wote wakawa sehemu ya Mfumo huu wa utawala unaojengwa na wasanii wenyewe kwa kuratibiwa na BASATA.

Sanaa ni Kazi Kwa Pamoja Tuikuze na Kuithamini.


Ghonche Materego
KATIBU MTENDAJI

No comments:

Post a Comment