Friday, December 30, 2011

MTANGAZAJI WA TBC TAIFA HALIMA MCHUKA AFARIKI DUNIA


Rais Jakaya Kikwete na mkewe, Mama Salma, wakimjulia hali aliyekuwa mtangazaji wa TBC Taifa, Halima Mchuka wakati wa uhai wake alipokuwa amelazwa hivi karibuni.

Halima amefariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya jana kuugua ghafla, alipoanza kujisikia vibaya mara tu baada ya kumaliza kipindi cha salam cha mchana na kupelekwa Hospitali.

Kufuatia kifo hicho, KLABU ya soka ya Simba ya Dar es Salaam inatoa salamu za rambirambi kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na tasnia ya habari kwa ujumla kufuatia kifo cha aliyekuwa mtangazaji maarufu wa michezo nchini, Halima Mchuka, aliyefariki usiku wa kuamkia leo
Jina la Halima Mchuka ni maarufu kwa wanamichezo si Tanzania pekee bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati kwa vile yeye aliweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kutangaza mchezo wa soka redioni.
Katika enzi za uhai wake, Halima alifanya kazi kwa karibu na klabu ya Simba, akitembelea ofisi za makao makuu mtaa wa Msimbazi kwa ajili ya kutafuta taarifa mbalimbali za kimichezo.

Simba itaukumbuka daima mchango wa Halima Mchuka kama mwanahabari, mwanamichezo na mtu ambaye alivutia wanawake wengi kupenda mchezo wa soka na pia kazi ya utangazaji na uandishi wa habari kwa ujumla.
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi. Amen.

Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga Ofisa Habari
Simba Sports Club
0772 01 72 47

No comments:

Post a Comment