Thursday, December 8, 2011

NBC yatoa changamoto, mafanikio miaka 50 ya uhuru


Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam

IMEELEZWA kuwa Tanzania bado inakabiliwa na uhaba wa huduma za kibenki na kukabiliwana changamoto kadhaa licha ya kuwepo mafanikio katika miaka 50 ya uhuru.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Lawrence Mafuru alisema kuwa wakati wa uhuru Tanganyika ilikuwa na benki moja tu ambayo ni Benki ya Taifa ya Biashara lakini baadaye kulijitokeza benki kadhaa ambazo zilichangia kwa kiwango kikubwa kukuza maendeleo ya taifa hili.

Alisema NBC kwa kiwango kikubwa ilichangia kukuza maendeleo ya taifa hili kwani ilishiriki kwa kiwango kikubwa katiuka ujenzi wa barabara na viwanda jambo ambalo lilichangia kwa kiwango kikubwa sana ukuaji wa maendeleo ya Tanzania.

Mafuru alisema kuwa nchi inaadhimisha miaka ya 50 ya uhuru lakini benki ya NBC itakuwa ikiadhimisha miaka 45 ya uwepo wake mapema mwakani jambo ambalo inaonesha ukomavu na ukongwe wa benki hii.

“Kuna mafanikio mengi sana ya kifedha ambayo tunajivunia licha ya nchi yetu kuendelea kutajwa katika kundi la nchi masikini kwa takwimu za kimataifa lakini ukweli ni kwamba tumeweza kusonga mbele kwa kiwango kikubwa sana katika masuala ya kifedha ukilinganisha nia miaka 50 iliyopita” alisema.

Alisema kuwa NBC imeweza kupiga hatua kubwa kwani mpaka hivi sasa ina matawi 53 nchini yaliyounganishwa katika mtandao wa teknolojia ya kisasa ya kibenki na kutoa huduma za kisasa zinazokidhi mahitaji kwa wateja yanayoendana na wakati.

NBC imeweza kutoa ajira za kudumu kwa wafanyakazi zaidi ya 1500 jambo ambalo limechangia ongezeko la kipato kwa watanzania na kupunguza tatizo la ajira nchini.

Pia Mafuru alisema kuwa NBC imekuwa mdau mkubwa wa huduma za kijamii hasa katika huduma za Afya, Elimu na uwekezaji katika makundi ya wasio na uwezo wa kumudu kupata huduma hizo muhimu nchini huku sulala la elimu peke yake NBC ikitumia kiasi cha shs Bilioni tatu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Halikadhalika Mafuru alisema kuwa NBC bado inaendelea kuwa mdau mkubwa katika maendeleo ya taifa kwani kwa sasa inachangia upatikanaji wa makazi bora kwa watanzania kwani hivi karibuni imeingia mkataba na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili kuweza kujenga makazi bora na ya bei rahisi kwa ajili ya watanzania.

Akizungumzia changamoto zilizopo nchini Mafuru alisema Tanzania bado inahitaji huduma za kibenki kwa kiwango kikubwa licha ya fikra ya kuwepo kwa changamoto baada ya kampuni za simu kujihusisha na utoaji wa huduma za kifedha, jambo ambalo alisema bado mahitaji ni makubwa sana. “Kwa sasa tuna benki 45 tu nchini ambazo zinatoa huduma kwa asilimia 10 tu ya watanzania hali hii inaonesha bado kuna mahitaji makubwa sana ya benki nchini hapa” alisema Mafuru.

Pia alisema hapa nchini kumekuwa na tatizo la kutokuwa na utamaduni wa uwajibikaji licha ya kuwepo wasomi wengi lakini bado taifa linahitaji watu wa kujitoa na kujituma zaidi katika utendaji wa kazi na kukuza weledi ili kuendana na wakati huu wa utandawazi, jambo ambalo limekuwa likitia hofu wengi kuwa nchi itakapoingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki watanzania wengi wanaweza kupoteza ajira hoja si kutokuwepo kwa wasomi ila suala lipo katika uwajibikaji.

Alisema ikiwa watanzania watajituma na kufanya kazi kwa bidii hakuna haja ya kuogopa kwani watakuwa na uwezo wa kushindana.

No comments:

Post a Comment