Saturday, January 21, 2012

MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AANZA ZIARA YA KISERIKALI MKOANI LINDI




Na Boniface Makene wa Ofisi ya Makamu wa Rais Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameanza ziara ya siku nne ya kiserikali mkoani Lindi leo Ijumaa Januari 20, 2012. Katika ziara hii Makamu wa Rais anatembelea wilaya za Nachingwea, Lindi na Kilwa. Hii ni mara ya kwanza kwa Dkt. Bilal kufanya ziara mkoani hapa akiwa Makamu wa Rais ambapo anapata fursa ya kukagua miradi ya maendeleo na kuhamasisha wananchi kujiendeleza katika kazi zao mbalimbali. “Nimefarijika sana kuwa katika mkoa huu, nimepokea mapokezi mazuri na nimefarijika sana kuna wananchi wa mkoa wa Lindi namna wanavyojitutumua katika kusaka maendeleo ya maisha yao,”alisema Dkt. Bilal siku ya kwanza ya ziara yake wakati akihutubia wananchi wa Chiumbali ambapo hapo kuna mradi mkubwa wa maji unatoka Masasi na unaolenga kutoa maji kwa wilaya za Masasi Nachingwea, mradi ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ukosefu wa maji katika Wilaya ya Nachingwea hasa nyakati za kiangazi. Kwa sasa wilaya ya Nachingwea iko katika hatua za kutanua kilimo na hali ya hewa wilayani hapa katika kipindi hiki inaonyesha kuwa upo uwezekano wa wilaya hii kupata mavuno mazuri ya mahindi ambayo yanaonyesha kustawi huku ardhi ya wilaya hii ikiwa na uwezo wa kumudu kuwa na mazao yenye rutuba bila kutumia mbolea za viwandani. Makamu wa Rais pia amekuwa katika shughuli za kuhamasisha ujenzi wa hosteli za wanafunzi hasa katika shule ya Nachingwea ambayo ni maalum kwa wanafunzi wa kike ambayo imeanzishwa mwaka huu na ina wanafunzi 50. Shule hii ina dhamira ya kuwa na michepuo ya sayansi na imejengwa kwa lengo la kukabiliana na tatizo la mimba kwa watoto sambamba na ndoa za utotoni. Mkoa wa Lindi unakabiliwa na changamoto nyingi na moja kubwa ni soko la zao la Korosho ambapo sasa wakulima wana shauku kubwa ya kupata malipo yao ya pili kufuatia mfumo wa stakabadhi ghalani, malipo ambayo hayajatolewa. Katika kukabiliana na tatizo hili Makamu wa Rais amemwagiza Waziri mwenye dhamana ya Kilimo na Ushirika kukutana na wadau wa zao la Korosho ili kujadiliana na kutoa jibu la tatizo hili katika kipindi kifupi kijacho, ili kuwapa wananchi hamasa ya kuendelea kuzalisha korosho. Makamu wa Rais pia anasisitiza juu ya wananchi kutumia demokrasia iliyopo nchini kwa kukosoa serikali huku wakibaini kuwa, demokrasia ina mipaka yake na kwamba wajadiliane kwa busara katika mijadala ya kutafuta Katiba mpya na mwisho watambue hawana eneo jingine duniani linalowathamini zaidi ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment