Friday, February 3, 2012

JESHI LINALOTAWALA NCHINI MISRI LATANGAZA SIKU TATU ZA MAOMBOLEZO


Jeshi linalotawala nchini Misri latangaza siku tatu za maombolezo ya watu zaidi ya watu 70 wamefariki kufuatia ghasia kati ya mashabiki wa timu mbili katika mji wa Port Said, nchini Misri.

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya MISRI ambayo imeeleza kuwa Watu hao walikufa baada ya mashabiki kuanza kuingia uwanjani, baada ya mechi kati ya vilabu viwili vikuu vinavyoongoza ligi nchini humo, Masry na Al-Ahly, siku ya Jumatano.

Inahofiwa kwamba idadi ya vifo huenda ikaongezeka, kwani zaidi ya watu 156 wamejeruhiwa kati ya waliokufa ni pamoja na maafisa wa usalama.
Ukosefu wa usalama mkali ambao hudumishwa kwa kawaida huenda ikawa ni jambo ambalo lilichangia kutokea ghasia hizo.

Polisi nchini Misri wametulia mno tangu kufanyika maandamano yaliyomtoa Rais Hosni Mubarak madarakani.
Katika mechi hiyo ya Jumatano, timu ya Port Said, Masry, ilipata ushindi wa magoli 3-1.

Walioshuhudia walielezea kwamba kulikuwa na hali ya wasiwasi muda wote wa mechi hiyo, tangu shabiki mmoja wa Al-Ahly alipoinua bango ambalo inadaiwa lilikuwa linawatukana mashabiki wa timu ya nyumbani.

Maafisa wachache wa polisi walijitahidi kuwapa ulinzi wachezaji, lakini hawakufanikiwa kabisa na Sehemu moja ya uwanja ilichomwa moto.

Maafisa wanaohusika wameelezea kwamba vifo vingi vilitokana na watu kupata majeraha makubwa ya kichwa kwa kupigwa au kukatwa, na wengine kuzimia hadi kufa wakati wa mkanyagano.

Mechi zote za ligi kuu zimefutiliwa mbali, na bunge jipya la Misri linakutana leo katika kikao cha dharura kuujadili msiba huu.

No comments:

Post a Comment