Wednesday, February 22, 2012

Tamasha lahamishiwa Dodoma badala ya Mwanza






MWENYEKITI wa Tamasha la Pasaka, Alex Msama amesema kuwa, tamasha hilo limepangwa kufanyika Aprili 9, katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Akizungumza jijini leo, Msama alisema kuwa, kamati imeamua kulihamishia tamasha hilo mkoani Dodoma badala ya Mwanza, baada ya kuridhika na maombi ya wadau wa muziki huo.

"Kamati kazi yake kubwa ni kupokea maoni kutoka kwa wadau na kuyafanyia kazi, wajumbe wameamua lifanyike mkoani Dodoma badala ya Mwanza," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa, awali tamasha hilo lilipangwa kufanyika mkoani Mwanza, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Aprili 9, mwaka huu.

"Ni kitu cha kawaida kuhamisha sehemu moja kwenda sehemu nyingine, maamuzi ya kamati ni ya kuyaheshimu," alisema.

Mwaka jana, tamasha hilo lilifanyika katika mikoa mitatu, Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza.

Pia, Msama alisema kutokana na tamasha hilo kuwa la kimataifa, amewataka wafanyabiasha kujitokeza kudhamini tamasha hilo kubwa nchini.

Mpaka sasa, baadhi ya waimbaji nyota wa ndani na nje ya nchi wamethibitisha kushiriki, lakini kwa sasa wanaendelea na taratibu za kupata kibali cha kufanya kazi.

"Tayari baadhi ya waimbaji nyota wa ndani na nje waliopelekewa mialiko, wamethibitisha kushiriki, kilichobaki ni kushughulishia vibali vyao," alisema.

"Bado tunapokea maoni kutoka kwa wadau wetu, tunaomba mzidi kututumia ili tuyafanyie kazi kabla ya tarehe ya tamasha hilo," alisema.

Tamasha la Pasaka mwaka huu litafanyika Aprili 8, mwaka huu jijini Dar es Salaam na Aprili 9 litafanyika mkoani Dodoma. Kwa hisani ya blog ya majuto balile

No comments:

Post a Comment