Monday, February 13, 2012

WATU MILIONI MOJA KUFAIDIKA NA TAMASHA LA PASAKA BAADA YA MIAKA 20


NA SAMIA MUSSA

wa dira ya mtanzania

ZAIDI ya watu milioni moja wenye matatizo wanatarajia kufaidika na Tamasha la Pasaka litakapotimiza miaka 20, tangu kuanzishwa kwake na kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa tamasha hilo, Alex Msama, alisema tamasha hilo limelenga kiwasaidia watanzania, hivyo limekusudia kuwasaidia watanzania milioni moja kwa kuwapatia misaada mbalimbali.

Walengwa katika misaada hiyo ni wasiojiweza, walemavu, wajane na watoto yatima ambao wanasaidiwa fedha za ada na matumizi mbalimbali ya shule.

Msama alisema lengo lake kubwa la tamsha hilo litakapotimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, watanzania wasiopungua milioni moja wawe wamenufaika nalo, ambapo mwaka huu ni la kimataifa.

“Tusiitegemee Serikali kwa kila kitu, haiwezi kumsaidia kila mtu, vitu vingine tunatakiwa tufanye wenyewe kwa ajili ya kusaidia wenzetu kupitia vyanzo mbalimbali kama hili tamasha,” alisema.

Msama alisema kuwa, maandalizi ya tamasha la mwaka huu yanaendelea vizuri, ambapo tayari wamepatiwa kibali na litafanyika sehemu ya wazi ili liweze kushuhudiwa na wadau wengi wa muziki huo.

Licha ya maandalizi kuanza mapema, Msama alisema tamasha hilo la kimataifa litawahusisha waimbaji wa muziki huyo wa kimataifa ambao watatangazwa hapo baadaye.

Msama aliwataka waimbaji wazawa kuhakikisha mwaka huu, wanatumia vyombo vya muziki moja kwa moja, kwani suala la CD linaweza lisitumiwe.

“Wasanii mwaka huu watakuwa wengi zaidi ya mwaka jana, nawaomba waimbaji wa nyumbani wasitumie CD, kama ilivyokuwa mwaka jana nusu nzima ya wasanii walitumia,” alisema

Mbali ya mandalizi hayo kuendelea, wamekuwa na wakati mgumu kuamua tamasha hilo lifanyike mkoa gani kwasababu mikoa kama Mbeya, Kilimanjaro, Mwanza na Morogoro imeomba baada ya kufamnyika Jijini Dar es Salaam Aprili nane lihamie huko.

“Hatujajua litaelekea wapi baada ya Dar es Salaam, ila tuko katika mazungumzo kuona lifanyike mkoa gani kati ya mikoa hii iliyoomba baada ya siku chache tutatoa taarifa rasmi litaendelea wapi,” alisema

No comments:

Post a Comment