Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, March 7, 2012

'Aliyevua Kiatu' na Rose Muhando kutumbuiza Pasaka


Na Mwandishi Wetu MWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili nchini Kenya, Anastazia Mukabwa, naye amethibitisha kuwa miongoni mwa watakaotumbuiza katika tamasha la Pasaka litakalorindima Dar es Salaam Aprili 8 mwaka huu, pia katika Mkoa wa Dodoma. Mwenyekiti wa Kamati ya Msama Promotions, waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama alisema Dar es Salaam jana kuwa Mukabwa aliyeimba kwa kumshirikisha mwimbaji galacha wa Tanzania, Rose Muhando katika wimbo wa Vua Kiatu, ameahidi kukonga nyoyo za mashabiki. "Mpaka sasa tunaendelea na mazungumzo na waimbaji mahiri wa muziki wa Injili, lakini Mukabwa amethibitisha kushiriki na ataambatana na kundi la wanamuziki wake wanane," alisema Msama. Mukabwa bado anatamba na albamu ya Vua Kiatu aliyomshirikisha Muhando, na Msama amesema yuko kwenye mazoezi makali kujiandaa kufanya mambo makubwa. Albamu ya Vua Kiatu ina nyimbo nane ambazo ni Vua Kiatu uliobeba jina la albamu hiyo, Ee Mungu, Usiwe Manamba, Nzizilela, Nishike Mkono Bwana, Wanaokudharau na Mfalme. Mbali na Mukabwa, wengine waliothibitisha kushiriki tamasha hilo litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka ni Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho wa Dar es Salaam, kundi la Glorious Celebration na Atosha Kissava kutoka Iringa. Kwa mujibu wa Msama, tamasha hilo baada ya kufanyika Dar es Salaam, pia litarindima kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu. Tamasha la mwaka huu malengo yake makubwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji wanawake wajane. Kiingilio katika tamasha hilo zimetengwa katika kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti maalumu sh. 10,000. Tamasha la Pasaka la mwaka huu pia litashirikisha waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi sita za Afrika ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia. Pia kutakuwa na kwaya.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...