Friday, March 16, 2012

KAJALA KIZIMBANI

MSANII wa filamu nchini Kajala Masanja na mumewe
Faraja Chambo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa
na mashtaka matatu likiwemo la kula njama, kuhamisha umiliki wa nyumba na
kutakatisha fedha haramu. Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi,
Sundi Fimbo, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Leonard Swai alidai kuwa mwaka 2010 , Kajala na Chambo walikula
njama ya kuhamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi Salasala wilaya ya
Kinondoni kinyume na kifungu cha 34 cha sheria ya rushwa ya mwaka 2007 sura ya
11. Swai alidai kuwa Aprili 14, 2010 jijini Dar es Salaam washtakiwa hao kwa
pamoja kinyume na kifungu cha 34 (2)a(3) cha sheria ya kuzuia na kupambana na
rushwa walihamisha umiliki wa nyumba hiyo iliyopo Kunduchi Salasala jijini Dar
es Salaam. Alidai kuwa siku hiyo ya Aprili 14,2010 washtakiwa hao ambao ni mtu
na mkewe walifanya uhamisho wa umiliki wa nyumba hiyo iliyopo Kunduchi Salasala
ambayo ilipatikana kutokana na fedha haramu. Wakati kesi hiyo ikiendelea Kajala
pekee ndiyo aliyokuwepo mahakamani hapo na mumewe Chambo ambaye anakabiliwa na
kesi nyingine za kutakatisha fedha haramu mahakamani hapo hakuwepo. Katika kesi
hiyo, Kajala anatetewa na Wakili Alex Mgongolwa ambaye alidai mahakamani hapo
kuwa Wakili huyo wa Takukuru , Swai hana mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na
kwamba hati ya mashtaka inamapungufu. Akijibu hoja: Wakili Swai alidai kuwa
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliteua mawakili wa Takukuru chini ya Government
Notice (GN) 168 ya mwaka 2010 na kuwaruhusu kuendesha kesi zisizokuwa za rushwa
na kwamba katika uteuzi huo yeye alikuwa ni mmojawapo. Hivyo anauhalali wa
kuendelea kuendesha kesi hiyo. Hakimu Fimbo ameiahirisha kesi hiyo hadi Aprili
20, mwaka huu atakapotoa uamuzi juu ya hoja hizo.
HABARI KWA HISANI YA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment