Joshua Nasari |
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) amesema sasa yuko tayari kufunga ndoa na Mbunge mteule wa chama hicho wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.
“Nafurahi kwamba Nassari hatimaye ameshinda ubunge katika uchaguzi mdogo,” alisema Mdee wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Arusha na Meru juzi katika viwanja vya Leganga kusherehekea ushindi wa chama chake katika uchaguzi huo.
Mdee alifafanua, kwamba yeye na chama chake walikuwa wamebanwa na kampeni za kuhakikisha Chadema inatwaa jimbo la Arumeru Mashariki na ndiyo sababu hakujibu mara moja maombi ya Nassari ya kumwoa aliyoyatoa katika moja ya mikutano yake ya kampeni.
“Naondoka kwenda Dar es Salaam kujiandaa kwa Mkutano ujao wa Bunge, kisha nitakwenda Dodoma ambako nitamsubiri Nassari na kwa pamoja tutafanya maandalizi,” alisema Mdee huku akishangiliwa na hadhira hiyo huku wakiimba na kucheza katikati ya mvua iliyokuwa ikinyesha.
Mdee alisema ndoa kati ya wabunge hao wawili wa Chadema ni wazo zuri na itatangazwa sana na kuandika historia.
Alipoona anashambuliwa sana na wapinzani wake juu ya useja wake katika kampeni hizo, Nassari hatimaye alitangaza kumwoa Mdee ambaye pia hajaolewa.
Na katika moja ya mikutano ya hadhara, alisimama naye jukwaani kukampeni.
“Kuna viongozi wengi wa kidini Dodoma, ikiwa ni pamoja na ndani ya Bunge ambao watatushauri jinsi ya kulitimiza hili,” alisema Mdee na kuongeza kwamba baba yake Joshua, Mchungaji Samuel Nassari alipata kusema, ‘mwanamke mzuri ni zawadi kutoka kwa Mungu’.
Chadema ina idadi kubwa ya wabunge vijana ambao hawajaoa, ikiwa ni pamoja na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Mr Sugu’; wa Ubungo, John Mnyika; wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na sasa Nassari.
Halima Mdee |
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ametaka wananchi kutoa maoni ya Katiba mpya ili walete mabadiliko mwaka 2015.
Aidha, amewasihi kuacha kutopiga kura, kwa kuwa katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki waliojitokeza walikuwa wachache.
Aliwasihi vijana kujitokeza Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakapotolewa kwa ajili ya kuboresha taarifa zao na wengine kujiandikisha upya.
Alisema hayo katika mkutano huo na kumsifu Nassari ambaye alidai ni kijana atakayeleta mabadiliko ndani ya jimbo hilo ingawa baadhi ya watu walihoji umri na mambo mengine. Mbowe alisema chama hicho kitatumia njia ya miguu, magari hata helikopta nchi nzima, kufikia wananchi ili watoe maoni yao juu ya mchakato wa Katiba mpya.
Alitoa rai kwa Polisi kuacha kupiga mabomu, kutumia risasi na nguvu zaidi, nyakati za uchaguzi kwani vijana wanaoumia ndio watakaokuwa viongozi wa baadaye.
"Nawashukuru kwa kunipa kijana mjanja, yaani Nassari namkabidhi Lema (Godbless) ili aje naye mjengoni (bungeni) na sisi wabunge wa Chadema tutampokea na wananchi.
“Lakini nawapasha ninyi vijana, kunapotokea suala la uamuzi wenu kwa ajili ya maendeleo, pigeni kura na natoa rai, tumieni marekebisho ya Daftari mjiandikishe na kulinda kadi zenu, ili tulete maendeleo, kwani ushindi wa Chadema ndiyo safari ya CCM mwaka 2015 na kila wanapotupiga mabomu tunashinda," alidai Mbowe.
Mbunge wa Arusha Mjini, Lema alishukuru wananchi hao na kusema watuhumiwa wa rushwa wakae chonjo, kwani baada ya Chadema kushinda Arusha Mjini na Arumeru Mashariki maendeleo yatapatikana.
Aliomba wananchi kuondoa itikadi zao za vyama na kumpa ushirikiano Nassari kwa kuwa yeye ndiye mbunge atakayewaletea maendeleo. Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa, alisema ushindi huo ni wa kishindo, kwani walimtanguliza Mungu na kutoa angalizo kuwa jimbo la Monduli nalo wanakaribia kulichukua.
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo alisema yeye si mtu wa ahadi hewa, hivyo atashirikiana na Nassari kuchimba visima viwili na kuongeza kuwa mfadhili wa chama hicho, Mustapha Sabodo, amejitolea kuchimba vinne ili kuondoa kero ya maji jimboni humo.
Habari: Gazeti la Habari Leo.
Habari: Gazeti la Habari Leo.
No comments:
Post a Comment