Thursday, April 5, 2012

ZIDANE AWAHIFADHI SIMBA ALGERIA



Hoteli la Zidane
KIKOSI kamili cha Simba kimewasili jijini Setif leo majira ya saa saba na nusu mchana saa za hapa (saa tisa na nusu saa za huko), baada ya safari ndefu ya kutoka Algiers.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema kutoka mjini Setif kwamba klabu yake iliwasili Algeria jana lakini ilishindwa kwenda Setif kutokana na kukosa usafiri wa ndege, na kukataa usafiri wa basi ulioandaliwa na wenyeji wao.
Wakati wenyeji wakidai kwamba usafiri wa kutoka Algiers ilikolala Simba hadi Setif ni masaa matatu, leo Simba imetumia takribani dakika 45 kwenda mji wa Bizaya (Bezaia) kwa usafiri wa anga na kisha kupanda basi kwa muda wa karibu masaa mawili na nusu hadi kufika Setif.
Kwa kawaida, usafiri wa ndege nchini Tanzania muda wa dakika 45 hutosha kumfikisha mtu mkoani Arusha kwa usafiri wa anga akitokea Dar es Salaam na hivyo viongozi wa Setif walikuwa wakisema uongo walipodai kuwa safari ya basi ingetumia muda wa masaa matatu.
Kama Simba ingefuata ushauri wa Setif jana, ni wazi kuwa ingeingia katika mji huu usiku na isingeweza kufanya mazoezi siku ya jana.
Hata hivyo, msafara wa Simba chini ya Mwenyekiti Ismail Aden Rage, ulisimama kidete na kuamua kulala Algiers jambo lililosaidia timu kufanya mazoezi jana.
Wekundu wa Msimbazi wamefikia katika Hoteli ya Zidane iliyopo katikati ya mji wa Setif na kuna taarifa kuwa hoteli hiyo ni miongoni mwa vitega uchumi vya mwanasoka bora wa zamani wa dunia, Zinedine Zidane, Mfaransa mwenye asili ya Algeria.
Jana Simba ilifanya mazoezi yake katika uwanja wa kijeshi jijini Algiers chini ya ulinzi mkali kwa muda wa masaa mawili.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika benchi la ufundi la Simba leo klabu itafanya mazoezi yake katika Uwanja wa Mei 8, 1945 majira ya saa 12 jioni kwa saa za hapa.
Uwanja huo ndiyo utakaotumika kwa ajili ya mechi ya Kombe la CAF baina ya Simba na Setif iliyopangwa kufanyika keshokutwa saa 12 jioni kwa saa za hapa sawa na saa mbili usiku kwa saa za Tanzania.
Msafara wa Simba umekuwa kivutio kikubwa nchini Algeria, kutokana na unadhifu wa wachezaji wake ambao wote wamevaa suti za wabunifu zinazowatofautisha na abiria wote wengine kwenye viwanja vya ndege ambako timu imepita.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Algeria, mechi ya keshokutwa itachezeshwa na waamuzi kutoka Tunisia huku Kamisaa wa mchezo akiwa anatokana nchini Gabon.

No comments:

Post a Comment