Herieth Makwetta, gazeti la Mwanaspoti
MSANII anayeongoza nchini Tanzania kwa
ubunifu wa kufanya shoo nzuri na zenye mvuto mkubwa kwa mashabiki wake amesema
kuwa kwake muziki ni ajira na ni kazi kama ilivyo kwa mfanyakazi anayeingia
ofisini.
Mshindi huyo wa tuzo tatu za Kilimanjaro
kwa mwaka huu na mwaka 2010, alisema kuwa anafanya kazi hiyo kwa malengo zaidi
na ndio maana anaweza kuwateka mashabiki wake na kuufanya muziki wa kizazi
kipya uzidi kupendwa ndani na nje ya nchi.
"Nafanya muziki kama kazi, sifanyi
muziki kujifurahisha mimi na kutafuta pesa pekee huku nikiwaacha mashabiki
zangu hawajakata kiu ya burudani," alisema Diamond.
Alisema kikubwa hasa anachokifanya ni
kushirikiana na watu na siku zote anaamini kuwa hawezi kufanya kazi peke yake
pasipo kuwa na wacheza shoo wake kwani ndio wanaompa sapoti kubwa na
kubadilishana mawazo ili kuleta vionjo vipya.
"Unajua mimi sina ubahili hasa
ninapofanya kazi, na hili ndilo lililonifanya nizidi kusonga mbele katika kazi
ya muziki ili upate ni lazima utoe, ili nifurahishe mashabiki ni lazima
nizingatie kanuni kama hizi," alisema.
Diamond aliongeza kuwa maandalizi ni silaha
nyingine ambayo inamfanya kila siku mashabiki wamwone mpya. "Siwezi
kutokeza machoni mwa mashabiki nikiwa hivyo hivyo kila siku hata nikiwa na
wimbo mpya sidhani kama watanifurahia kila siku staili hizo hizo, pia
namtanguliza Mungu katika kila jambo," alisema.
Hata hivyo amewashukuru mashabiki na
kuahidi kutowaangusha "nawashkuru sana na nawaahidi kuwa sitowaangusha na
wategemee vitu vipya".
Wikiendi iliyopita msanii huyo alifanya
shoo katika sehemu ya kiburudani ya Dar Live iliyopo jijini Dar es Salaam na
kuvunja rekodi kwa kuingiza mashabiki wengi zaidi kuliko shoo zote zilizowahi
kufanyika sehemu hiyo
Diamond ambaye alivaa mavazi ya kibaharia
aliwasili eneo hilo kwa usafiri wa helikopta na hatimaye kuingia katika gari
aina ya benzi ambalo lilimsogeza mpaka jukwaani.
Licha ya mvua kubwa iliyonyesha mashabiki
walionekana kujifunika viti vyao kichwani ili waweze kuona utumbuizaji wa
msanii huyo.
|
No comments:
Post a Comment