Mchoraji wa katoon magazeti ya The Guardian Muhidin Msamba,
akimzawadia Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Zawadi ya picha ya kuchora
wakati wa mafunzo hayo.
Leo TGNP imezindua warsha ya uraghbishi ya wiki moja
kwa wanaharakati kutoka mikoani pamoja na Dar es Salaam, ili kunoa
uwezo wao wa kufanya kazi na jamii husika kuibua masuala nyeti
katika jamii hizo zikiwemo mafanikio na changamoto, kuchambua visababishi
vya matatizo au mafanikio hayo kwa kina na kupanga mikakati ya
kushughulikia kero hizo pamoja na wanajamii .
Warsha hiyo inalenga kuimarisha uelewa wa pamoja wa mtizamo
ya kiitikadi kuhusu dhana za ukombozi wa wanawake
kimapinduzi na makundi yaliyoko pembezoni na kuitekeleza
kwa vitendo; kujenga uelewa wa pamoja kuhusu
uraghbishi na mbinu shirikishi zinazotumika katika
uraghbishi, kuongeza uelewa wa kampeni ya hiaki ya uchumi
katika kudai kazi zenye heshima utu na kipato, uhifadhi wa kumbukumbu,
mbinu za mawasiliano na uwezo wa kuvitumia katika Ujenzi
wa Vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi ya
kanda.
Wawezeshaji wa warsha hiyo ni Bw. Richard Mabala
Mkurugenzi wa TAMASHA ambayo ni asasi ya kiraia iliyobobea
katika kuwawezesha vijana na jamii kwa ujumle kutumia mbinu
za uraghbishi kama chachu ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii
husika. Bw. Winston Chuchil Mkurugenzi Msaidizi wa TAMASHA ni
mwezeshaji mwenza ambaye naye pia amebobea katika mbinu za uraghbishi.
Washiriki wa Warsha hiyo wametoka katika mikoa ya Shinyanga, Morogoro,
Arusha, Dodoma, Mwanza , Mbeya, Dar es Salaam na Pwani wakiwakilisha
asasi mbalimbali za kiraia ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuleta
mabadiliko chanya katika jamii za mikoa husika.
Baada ya warsha washiriki wakishirikiana wanajamii na
TGNP wataendesha zoezi la uraghbishi katika mikoa husika ambapo
watatumia mbinu mbali mbali za uraghbishi katika kuibua
masuala nyeti yanayogusa jamii husika, kuyachambua kwa kina ili kupata
kiini cha matatizo au mafanikio, hayo na kutafuta mbinu
mbali mbali za kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo, mbinu zitakazotumika,
nani atafanya nini kuanzia ngazi binafsi, jamii na taifa.
No comments:
Post a Comment