(TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI)
TUZO YA MWANAMICHEZO BORA WA TANZANIA
CHAMA
cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) Jumapili Mei 20,
2012 saa nne asubuhi kitatangaza mdhamini wa Tuzo za Mwanamichezo Bora
wa Tanzania kwa mwaka 2011.
Mdhamini
huyo atatangazwa kwenye mkutano ambao ataufanya Mwenyekiti wa TASWA,
Juma Pinto pamoja na mdhamini wa tuzo hizo, ambapo mkutano huo
utafanyika kwenye mgahawa mpya uitwao City Sports & Lounge uliopo
jirani na mnara wa askari makutano ya barabara ya Samora na Azikiwe,
Posta Dar es Salaam.
TASWA
inachukua fursa hii kuwaalika waandishi wote wa habari za michezo
kuhudhuria kwenye mkutano huo ili tuweze kuanza pamoja katika mbio hizi
za kuelekea kwenye Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Mwaka 2011.
Tayari
Kamati ya Tuzo ishateuliwa na imetangazwa, hivyo baada ya mkutano huo
taratibu nyingine zitatangazwa kwa kadri zitakavyokuwa zimekamilishwa na
Kamati
Maalum ya Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Tanzania.
Kwa
miaka mitano iliyopita walioshinda Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA
walikuwa ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007), Mary Naali
(2008), ambao wote ni wanariadha, wakati 2009 na 2010 alikuwa mcheza
netiboli Mwanaidi Hassan.
KIFO CHA
MAFISANGO
TASWA
imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha kiungo wa timu ya
Simba ya Dar es Salaam na mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi),
Patrick Mutesa Mafisango kilichotokea alfajiri ya Alhamisi kwa ajali
ya gari jijini Dar es Salaam.
TASWA
inatoa pole kwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage, wachezaji wa timu
hiyo, mashabiki na Watanzania kwa ujumla kutokana na msiba huo mkubwa
kwa familia ya mpira wa miguu.
Tunaamini
waandishi wa habari za michezo wameguswa kwa kiasi kikubwa na msiba
huo, kwani wakati wa uhai wake marehemu alikuwa na ushirikiano mkubwa na
wanahabari na hakuwa mtu mwenye maringo, kiasi cha kushindwa kutoa
ushirikiano kwa wenzake.
Tunasema
kifo chake ni pigo si kwa Simba na familia yake tu, bali hata kwa timu
ya Taifa ya Rwanda na Wanyarwanda wote, ambao pia tunawapa pole kwa
msiba huo.
Tunawapa
pole wanamichezo wote na kuwaomba wawe na subira na uvumilivu katika
kipindi hiki kigumu, huku wakiamini waandishi wa habari za michezo tupo
nao pamoja katika majonzi hayo na kumuomba Mungu aiweke roho ya marehemu
mahali pema peoni. Amina.
Kifo cha Mzee Limonga
Tunapenda
kuwajulisha waandishi wa habari za michezo wote pamoja na wadau wengine
kuwa mtangazaji wa habari za michezo wa Redio Uhuru, Limonga Justine,
amefiwa na baba yake mzazi jana Alhamisi asubuhi kwenye hospitali ya
Temeke, Dar es Salaam.
Msiba
upo Mbagala kwa Mangaya, Dar es Salaam na maziko yanatarajiwa kufanyika
kesho Jumamosi. Naomba tuungane naye mwenzetu katika kipindi hiki
kigumu kwake na tumfariji kwa kadri tuwezavyo kwa kuondokewa na mzazi
wake. Nambari yake ya simu ni
0713-604578.
No comments:
Post a Comment