Friday, May 11, 2012

Wanaume wazikimbia familia kwa kisingizio cha ugumu wa maisha





Mhariri Mkuu wa Mtandao wa Thehabari.com, Joachim Mushi (kulia) akifanya mahojiano na moja ya familia Kijijini Msasa, Wilaya ya Handeni hivi karibuni.
Na Joachim Mushi, Handeni
BAADHI ya wanaume wamelazimika kuzikimbia familia zao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha. Wanaume hao wamezitelekeza familia hizo na kuziacha na wake zao na wao kutokomea maeneo mbalimbali kusaka maisha.
Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni mjini hapa na mwandishi wa habari hizi kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) umebaini kuwepo na familia nyingi ambazo zimetelekezwa na wanaume kwa kisingizio cha kwenda kutafuta maisha maeneo mengine.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kwediyamba, Juma Abdul ambacho ni moja ya vijiji vyenye idadi kubwa ya familia zilizotelekezwa, alisema matukio ya utelekezaji familia kijijini hapo ni mengi na yamekuwa yakijitokeza kwa mitiozamo tofauti.
Alisema kijiji hico kina kaya nyingi zilizotelekezwa na wanaume, huku likiwepo kundi lingine la wanawake waliozaa watoto na wanaume bila kufunga ndoa na baadaye wanaume kutoweka kwa madai wamekwenda kutafuta maisha maeneo mengine.
Naye Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kidereko, Shaban Muya alisema matukio ya utelekezaji familia kwa kisingizio cha ugumu wa maisha hasa kwa vijana wanaoingia kwenye ndoa ni mengi katika kijiji hicho jambo ambalo limewalazimu kuanza kampeni ya kutaka wazazi wawawezeshe vijana wao wanapoingia kwenye ndoa.
“Ofisi yetu imekuwa ikipokea malalamiko kama hayo mengi na kuangalia namna ya kusuluhisha kulingana na imani zao…kama ni Waislamu yakitushinda hupeleka Ofisi za BAKWATA mjini Handeni na kama ni Wakristu huangalia taratibu za dini hiyo pia, lakini zipo familia zinatelekezwa ama wanatengana na wenza wao na mwanamke anaendelea kuhudumia familia bila kulalamika, eneo kama hilo viongozi hatuwezi kuingilia,” alisema Muya.
Vijiji ambavyo vimetembelewa na kushuhudia idadi kadhaa ya familia zilizotelekezwa ni pamoja na Kwediyamba, Kivesa, Msasa, Komnyang’anyo, Kidereko, Vibaoni na Kwachaga.
Naye Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii wilayani Handeni, Zawadi Gwando, alisema kesi za malalamiko ya utelekezaji familia eneo hilo ni nyingi jambo ambalo limeifanya idara hiyo kutumia muda mwingi kushughulikia migogoro ya utelekezaji familia.
“Vitendo vya utelekezaji familia vipo vingi, kwa kutwa unaweza kushinda ukipokea kesi za utelekezaji familia tu hadi mwisho wa kazi...tatizo asilimia kubwa ya wakazi wa mji huu ni Waislamu ambao unakuta wana wake zaidi ya mmoja...sasa inatokea mume anatelekeza baada ya kuona hali ngumu ya maisha,” alisema.
Hata hivyo, Bi. Gwando ameshauri mamlaka za sheria kuangalia upya sheria na adhabu zinazotolewa kwenye kesi za migogoro ya ndoa kwani adhabu nyingi haziendani na wakati jambo ambalo huenda linawapa kiburi watuhumiwa wa makosa kama hayo.
Uchunguzi umebaini baadhi ya watoto kutoka familia zilizotelekezwa wameshindwa kuendelea na masomo hasa ya Sekondari kwa kile mama kukosa kipato cha kutosha kuwasomesha watoto alioachiwa na mumewe.
 
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA).

No comments:

Post a Comment