Tuesday, June 12, 2012

BASATA: WASANII JIPANGENI KUHIMILI USHINDANI WA KIMATAIFA

Na Mwandishi Wetu
 
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kujipanga kwa ajili ya kuhimili ushindani wa kimataifa kutokana na ujio wa mfumo wa digitali ambao utazifanya kazi zao kuonekana kimataifa.

Wito huo umetolewa wiki hii kwenye ukumbi wa BASATA na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Ghonche Materego wakati akihitimisha mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa uliohusu Teknolojia ya Digital na Faida Zake Katika Sekta ya Sanaa uliochokozwa na Mhandisi Joel Chacha kutoka mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (Tcra).

Alisema kuwa, mfumo wa digitali utaruhusu uwepo wa vituo vingi vya redio na runinga ambavyo vitakuwa na masafa ya kimataifa hivyo ni wazi wasanii wanatakiwa kujipanga katika kuandaa maudhui bora, ya kutosha na yenye mvuto kwa ajili ya kukidhi ongezeko hilo na zaidi ushindani wa kimataifa.

“Wasanii tujipange, fursa zinazokuja ni nyingi mno, zinahitaji maudhui ya kutosha, yenye ubora na yatakayoweza kuvifanya vyombo vya habari viweze kuhimili ushindani pia” alisisitiza Materego.
Aliongeza kuwa, moja ya eneo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wamiliki wa vyombo vya habari ni uhafifu wa maudhui ya kazi za Sanaa hivyo, wasanii hawana budi kuacha kulalamika na kujipanga kukabili changamoto hiyo.
Awali akiwasilisha mada hiyo,Mhandisi Chacha alisema kuwa, mfumo wa digitali utazalisha fursa nyingi katika sekta ya Sanaa lakini akasisitiza kuwa, uchangamfu wa Wasanii wetu ndiyo utawafanya wafaidi.
Alizitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na; ongezeko la ajira kwa Wasanii, ongezeko la vipindi, kukua kwa ushindani katika ubunifu na utengenezaji maudhui yenye ubora, Sanaa za Tanzania kutangazika kimataifa na kuongezeka kwa makampuni yatakayojihusisha na sekta ya Sanaa

No comments:

Post a Comment