Tuesday, June 19, 2012

NHIF yamlilia Mhariri Mkuu Jambo Leo


Marehemu Willy Edward akipokea zawadi kwa Mshindi yake kama mshindi wa Ujumla wimbo wa Jojina
 
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umepokea kwa masikito makubwa kifo cha Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo, Willy Edward Ogunde ambaye alikuwa ni miongoni mwa wadau muhimu wa Mfuko huo.
 
Willy Edward enzi za uhai wake alitoa kipaumbele katika kuuhabarisha umma kwa kutoa habari zinazohusiana na sekta ya Afya hususan za kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
 
Mfuko utaendelea kukumbuka na kuenzi yote yaliyofanywa na Willy kupitia nafasi yake ya uhariri katika gazeti la Jambo Leo.
 
Marehemu kwa mara ya mwisho alihudhuria mkutano wa saba wa waandishi waandamizi na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika mjini Morogoro mkutano ambao hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwaelimisha juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mfuko.
 
Kutokana na hayo, wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wanaungana na tasnia ya habari, familia, ndugu na jamaa kuomboleza msiba wa mhariri huyo.
 
Akimzungumzia marehemu, Ofisa anayeshughulikia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), Athuman Rehan, alisema kuwa marehemu alikuwa ni mtu mtulivu na aliyependa kushirikiana na wenzake kwa hali na mali hivyo kuondoka kwake ni pigo kubwa kwa tasnia ya habari.
 
Katika kufanikisha shughuli za msiba, Mfuko umetoa rambi rambi yake kupitia uongozi wa Jambo Leo. Mungu ailaze roho yake pema poponi amina.

No comments:

Post a Comment