Napenda kuwatangazia wana-Bumbuli kwamba ile ahadi
niliyotoa wakati wa kampeni – ahadi ya kuanzisha Shirika la Maendeleo
Bumbuli – imetimia. Shirika limepata usajili, limefungua ofisi,
lina watumishi wa mwanzo na tayari ipo miradi minne ambayo utekelezaji
wake utaanza mara moja. Tutazindua Shirika hili tarehe 4 Agosti 2012,
katika mkutano wangu na wana-Bumbuli waishio Dar es Salaam na mikoa
ya jirani, na baadaye katika mikutano na wananchi jimboni Bumbuli.
Chimbuko
Nilipoamua kugombea
Ubunge wa Bumbuli mwaka 2010, niliamua kwamba katika utumishi wangu
kama Mbunge nitashirikiana na Wana-Bumbuli pamoja na marafiki na washirika
wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi katika kuleta mageuzi ya kiuchumi
na kijamii Bumbuli. Jimbo letu ni kati ya majimbo yaliyo nyuma kimaendeleo
kwa kiasi kikubwa na hivyo kuhitaji jitihada za ziada – zaidi ya zile
za Serikali. Katika kufikia lengo hilo, niliahidi kuanzisha Shirika
litakaloratibu shughuli za maendeleo katika Jimbo.
Nilifikia uamuzi wa
kuanzisha Shirika nikitambua kwa dhati uwepo wa jitihada nzuri
za serikali katika kuboresha maisha ya watu wa Bumbuli nikitegemea pia
serikali kuendeleza jitihada zaidi. Hata hivyo natambua kwamba kazi
ya maendeleo si kazi ya serikali pekee, inahitaji ushiriki wa kila mmoja
na hasa sekta binafsi ili kuisadia juhudi za serikali kufikia malengo
ya maendeleo. Nilitaka kuchambua uwezo wa watu binafsi, wafanyabiashara
na taasisi mbalimbali katika kupanua wigo wa ajira na shughuli za kipato
kwa watu wa Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii.
Mpango wa Mageuzi Bumbuli
Mpango huu ulitokana
na mawazo niliyokuwa nayo nilipoamua kugombea ubunge juu ya haja kuunganisha
jitihada za wenyeji wa Bumbuli, wafanyabiashara na taasisi za hapa nchini,
na wawekezaji kutoka nje katika kufanikisha mageuzi ya kijamii na kiuchumi.
Niliamini jitihada za sekta binafsi zikioana na mipango ya maendeleo
ya serikali kutachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa wana-Bumbuli na
hivyo kupanua wigo wa ajira na shughuli za kibiashara za uzalishaji
mali katika Jimbo.
Malengo ya mpango wa
kuikwamua Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii ni kama ifuatavyo:
- Kuongeza pato la wakulima wa Bumbuli kutokana na mazao wanayovuna kwa kuboresha mbinu za kilimo, mbinu za kuhifadhi mazao, na hatua mahsusi za kuongeza thamani ya mazao hayo (value-addition).
- Kuwavutia wawekezaji kujenga taasisi au shule itakayokuwa na wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine watakaotumia bidhaa zinazozalishwa Bumbuli, hivyo kutengeneza ajira na fursa za kujiongezea kipato kwa wananchi.
- Kuleta huduma za kifedha kwa kuanzisha taasisi ya fedha Bumbuli ambayo hatimaye itakuwa benki ya wananchi wa Bumbuli ambayo itatoa mikopo kwa masharti nafuu.
- Kuchukua hatua mahsusi za kuhifadhi mazingira ya Milima ya Usambara kwani maisha na maendeleo ya kiuchumi ya watu wa Bumbuli yanategemea sana mazingira na mandhari ya milima ya Usambara.
- Kuanzisha Shirika la Maendeleo Bumbuli litakalokuwa na jukumu la kubuni, kuratibu na kusimamia uendeshaji wa shughuli zilizoainishwa hapo juu. Shirika hili ndilo litakalokuwa kiini cha mtandao wa kijamii wa uchumi kwa Bumbuli.
Malengo haya yamekusudiwa
kuwanufaisha wananchi kwa kuanzisha mtandao wa kimataifa wa kibiashara
ambapo wadau mbalimbali watashiriki; na hatamu za uchumi zikishikiliwa
na watu wa Bumbuli wenyewe.
No comments:
Post a Comment