Monday, August 13, 2012

Benki ya Exim yajipanga kuboresha Shule ya Msingi Kilakala


 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim Bw. Anthony Grant akikata utepe kuashiria makabidhiano ya madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni nane kwa Shule ya Msingi ya Kilakala iliyopo katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam jana. Kutoka kulia ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Abdul Kutarasa, Diwani wa Kata ya Kilakala, Elizabeth Magwaja (wapili kulia) na Afisa Elimu Manispaa ya Temeke, Angela Frank (wapili kushoto). Picha na Mpiga Picha wetu.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim Bw. Anthony Grant akiteta jambo na mmoja wa wanafunzi wa shule msingi Kilakala wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni nane kwa Shule ya Msingi ya Kilakala iliyopo katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam jana. Akishuhudia watatu kushoto ni Meneja Mkuu Msaidizi wa Benki y Exim N. Seshagiri Rao. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim Bw. Anthony Grant akisalimiana na mmoja wanafunzi wa shule msingi Kilakala muda mfupi kabla ya kukabidhi madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni nane kwa shule hiyo iliyopo katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi wetu

BENKI ya Exim Tanzania imetoa mchango wa madawati 100 yenye thamani ya shillingi milioni nane kwa shule ya Msingi ya Kilakala iliyopo Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya mchango wa benki hiyo kwa jamii.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi madawati hayo jijini Dar es Salalam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Anthony Grant benki inayosherehekea miaka 15 tangu ianzishe mwezi huu wa Agosti alisema benki inaelewa umhimu wa elimu katika maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Grant alitangaza kuwa benki yake itakuwa mlezi wa shule hiyo huku ikisema kuwa benki yake itakuwa mstari wa mbele kukabiliana na matatizo mbalimbali yaliyopo shuleni hapo.

Grant alisema kuwa pamoja na kutoa madawati 100, benki yake itaendelea kuisadia shule hiyo katika maeneo mbali mbali baada ya kufanya uchunguzi uliothibitisha kuwa shule inakumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa madawati.

“Leo hii tunatangaza mahusiano mapya baina ya Benki ya Exim na Shule ya Msingi ya Kilakala. Leo hii tunakabidhi madawati 100 lakini pia tutaendelea kuisadia shule katika maeneo mengine kwa awamu.

“Tunaimani kuwa mahusiano yetu yatahakikisha kuwa shule inakuwa katika mazingira mazuri ya kujifunzia. Tunatambua umuhimu wa elimu katika nyanja zote mbili za kijamii na kiuchumi na ndiyo maana tumeamua kutoa mchango wetu katika masuala mbalimbali ya kielimu,” alisema.

Bw. Grant alisema kuwa benki yake imeona umuhimu wa kujikita zaidi kwenye shughuli chache za kijamii ambazo zitaleta mabadiliko chanya badala ya kuelekeza misaada michache ya kifedha katika shughuli mbalimbali za kijamii.

“Tukisharidhika kuwa tumeshafikia lengo letu na shule imeshapata kila kitu muhimu, baada ya hapo tutaendelea na mradi mwingine kwa kutumia falsafa ileile,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo ya msingi Abdul Kuratasa aliepokea madawati hayo kwa niaba ya shule aliishukuru benki kwa msaada wake uliowafikia katika wakati muafaka na kuhaidi kuyatunza na kuyatumia madawati hayo vizuri.

“Tunafuraaha sana kuwa Benki ya Exim imeridhia maombi yetu. Tunaimani mahusiano yetu haya mapya yatatuwezesha kujenga mazingira mazuri ya kujifunzia,” alisema.

No comments:

Post a Comment