Monday, August 27, 2012

NAPE AIGOMEA CHADEMA ASEMA WATAPAMBANA MAHAKAMANI


Akataa kuomba radhi, asema tuhuma atazithibitisha  mahakamani
Amtaka Dk. Slaha kuandaa bilioni 3 na shilingi moja
Ni kwa kudai CCM inaingiza silaa nchini. 

NA MWANDISHI WETU
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amewataka Viongozi wa Chadema kwenda mahakamani haraka badala ya kusubiri kuombwa radhi kama walivyotaka ili kusafishwa dhidi ya madai ya chama chao kupewa mabilioni ya fedha na mataifa tajiri.

Aidha amemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Wilbrod Slaa, kuiomba radhi CCM la sivyo itamburuza mahakamani kudai fidia ya sh. bilioni 3 na shilingi moja, kwa kuituhumu uongo kwamba imeingiza silaha kutoka nje  ya nchi tena bila kulipia ushuru.

Nape alisema hayo leo Agosti 27, 2012, kweneye mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba mjini Dar es Salaam.

"Bila shaka mmesikia jana Chadema wakinitaka niombe radhi au wananipeleka mahakamani kudai fidia ya sh. bilioni 3, kwa madai eti nimesema Chama hicho kinapata  mabilioni ya fedha kutoka kwa mataifa tajiri. 

Mkubwa hatishiwi nyau, nawataka waende haraka mahakamani wala wasisubiri hizo siku saba", alisema Nape.

Alisema, CCM inao ushahidi wa kutosha kuhusu madai aliyotoa Nape dhidi ya Chadema na kwamba huyo tayari kutoa uthibitisho huo mahakamani badala ya kuomba radhi.

"Nadhani wakienda mahakani itapendeza zaidi maana huko ndiko pazuri kutoa uthibitisho kuhusu tuliyosema, na ninawahakikishieni tukishathibitisha na Msajili wa Vyama akaupata uthibitisho huo chama chao kinafutwa", alisema.

Kuhusu CCM kumburuza Dk. Slaa mahakamani, Nape alisema, ameshawaagiza wanasheria wa Chama, kuandaa barua ya kusudio la mashitaka hayo, na Dk. Slaa atapelekewa ili aamue kama ataomba radhi au atakuwa tayari kwenda mahakamani.

"Wakati wanakwenda mahakamani, Chadema wamwambie babu yao ajiandae kuomba radhi au kuburuzwa mahakamani kuilipa CCM fidia ya sh. bilioni 3 na shilingi moja kwa kuizushia CCM uongo kwamba inaingiza silaha nchini tena", alisema Nape.

No comments:

Post a Comment