Friday, August 31, 2012

RIADHA TAIFA YAIPIGA KUMBO SIMBA VS AZAM NGAO YA JAMII



DAR ES SALAAM, Tanzania

MASHINDANO ya Taifa ya Riadha yanayotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia Septemba 7 hadi 9, yamelilazimisha Shirikisho la Soka nchini (TFF) kusogeza tena mbele hadi Septemba 11 kwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Azam FC itakayofanyika uwanjani hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa, jaribio lao la kukishawishi Chama cha Riadha (RT) kumaliza kwa wakati mashindano hayo katika siku ya mwisho ili kupisha mechi hiyo hapo Jumapili lilishindwa.

Kutoka na hali hiyo, TFF ilikubali matokeoa na kuamua kuisogeza mechi hiyo kwa mara nyingine hadi Jumanne alasiri, ambapo pambano hilo la kuashiria ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom linalohusisha bingwa wa ligi hiyo Simba dhidi ya mshindi wa pili ambayo ni Azam.

“Ligi Kuu sasa itaanza rasmi hapo Septemba 15, siku nne baada ya pambano la Ngao ya Jamii. Kanuni zinataka wiki moja kabla ya ufunguzi kupigwa kwa Ngao ya Jamii, lakini uwapo wa mashindano ya riadha umetulazimisha kufanya hivi. Tuna imani siku nne zitawatosha kujiweka tayari kwa ligi,” alisema Wambura.

Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Novemba 11, ambapo pambano gumzo baina ya mahasimu wa soka la Tanzania, Yanga na Simba zitacheza mechi ya kwanza baina yao hapo Oktoba 3 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Aliongea kuwa, katika mechi za pazia la ufunguzi wa ligi, mabingwa watetezu Simba watacheza na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku Polisi Morogoro na Mtibwa Sugar zikitoana ngao huko Jamhuri, Morogoro.

Ratiba hiyo inaonesha kuwa, Wajelajela waliorejea Ligi Kuu msimu huu Tanzania Prisons ya Mbeya siku hiyo itaoneshana ubabe na Yanga huko Sokoine, Mbeya, siku ambayo pia Mgambo JKT na Coastal Union zote za Tanga ziachuana huko Mkwakwani.

Mechi nyingine katika ufunguzi huo ni ile baina ya maafande wa JKT Ruvu na Ruvu Shooting watakaokipiga kwenye dimba la Chamazi Dar es Salaam, Kagera Sugar dhidi ya Azam FC  kwenye nyasi za Kaitaba, Bukoba, huku Toto Africans na Oljoro JKT wakioneshana kazi huko CCM Kirumba, Mwanza.

Ligi hiyo itamalizika Mei 18 mwakani kwa timu zote kujitupa dimbani, ambapo Toto Africans itafunga na Ruvu Shooting CCM Kirumba, Mgambo JKT dhidi ya African Lyon huko Mkwakwani, wakati JKT Ruvu itamaliza na Mtibwa Sugar KWENYE Uwanja wa Chamazi.

Miamba na mahasimu wa soka nchini Simba na Yanga watafunga msimu kwa pambano baina yao kwenye Uwanja wa Taifa, huku Tanzania Prisons itaumana na na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine, Oljoro JKT dhidi ya Azam huko Sheikh Amri Abeid na Polisi Morogoro dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa Jamhuri.

Aidha, Wambura aliongeza kuwa, endapo wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu barani Afrika, Simba na Azam hazitafanikiwa kuvuka hatua mojawapo ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, ratiba hiyo itafanyiwa marekebisho.

No comments:

Post a Comment