Thursday, August 16, 2012

WAZIRI MUKANGARA ATAKA RIPOTI YA OLIMPIKI 2012


Na Tullo Chambo
WAZIRI ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, imevitaka vyama ambavyo wachezaji wake waliiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olimpiki kuwasilisha ripoti kuanzia jinsi walivyojiandaa, kushiriki hadi matokeo waliyopata.
Agizo hilo limetolewa jana usiku na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo, katika hafla ya kuikaribisha timu ya Olimpiki ya Tanzania na kurejesha bendera ya taifa serikalini.
Akitoa maagizo hayo ya Waziri, Dk. Fenella Mukangara, Mkurugenzi huyo alisema waziri ameagiza viongozi wa vyama hivyo na vile vilivyokuwa katika mpango wa kusaka viwango vya kushiriki michezo hiyo, waandae tathmini ya ushiriki wao kupitia Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), na kuiwakilisha kwake.
“Viongozi wa vyama muandae tathmini ya ushiriki wenu wa Olimpiki, nini kimetokea ndani ya miaka  minne, mlifanya nini, mlikwama wapi na nini kifanyike,” alisisitiza Thadeo kwa niaba ya waziri, ambaye alikuwa akihudhuria vikao vya Bunge mjini Dodoma na kuongeza:
“Kama mlivyosema, maandalizi yanatakiwa yaanze kesho, sasa ili twende Brazil 2016 lazima tuwe tumejipanga kwa kutambua tatizo, kwa kufanya tahmini na kuweka mipango ya pamoja, ikiwashirikisha washika dau mbalimbali, si kwamba tunataka twende Brazil wakati vikwazo bado vipo palepale.”
Pia Mkurugenzi huyo aliwasilisha salamu za pongezi kwa wanamichezo hao, kwani kushiriki kwao kulitokana na kufuzu vigezo na wala si kupendeleana wala urafiki, hivyo wamejitahidi kwa kadiri ya uwezo wao, hivyo wakaribie nyumbani.
“Mheshimiwa Waziri, anawakaribisheni  na kuwapongeza sana, mmekutana na mengi sana ya ‘kuwa- discourage’ lakini mmepambana, mengi yametokea, hamkwenda huko kwa utashi wa mtu, mmepita katika vigezo, ni jambo la kujivunia, mmevipita vigezo na si urafiki, tuchukulie kama chachu, tukifanya vizuri tutapongezwa tu,” alisema.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Rais wa TOC, Ghulam Rashid, alisema matokeo hayo yametokana na aina ya maandalizi yaliyofanywa na vyama kwa kushirikiana na Kamati ya Olimpiki (TOC), huku akiwataka Watanzania kutambua kwamba ili kupata mafanikio katika mashindano ya kimataifa, inahitajika maandalizi na vifaa vya uhakika, vitu ambavyo viko juu ya uwezo wao, hivyo kila Mtanzania anatakiwa kusaidia kwa hali na mali.
“Tunaomba Watanzania waelewe, ili mchezaji afanye vizuri inahitajika maandalizi ya uhakika na ya muda mrefu na vyama vyetu ni malofa, haviwezi pekee yao, hivyo tunawajibu wa kuvisaidia ili viweze kuwaandaa vema na hatimaye kuja kufanya vema,” alisema Ghulam.
Katika Olimpiki London 2012, Tanzania iliwakilishwa na wanariadha, Samson Ramadhani ambaye alikuwa nahodha, Faustine Mussa, Zakia Mohamed na Msenduki Mohamed, ambaye hata hivyo hakukimbia baada ya kushikwa na nimonia, bondia Selemani Kidunda, waogeleaji Magdalena Moshi na Amaar Ghadhiar. Chanzo; Habari Mseto Blog

No comments:

Post a Comment