Thursday, August 16, 2012

WENGER: VAN PERSIE HAJAACHA PENGO, NILISHAZIBA KABLA


LONDON, England
 “Tayari tulishapata wa kujaza nafasi ya Van Persie kabla ya kumruhusu na kusema kweli sitarajii kusajili yeyote wa kumrithi, ninao wengi kikosini.”
 KOCHA Arsene Wenger wa Arsenal, amekiri kusikitishwa na maamuzi magumu aliyochukua ya kumuuza Robin van Persie kwa mahasimu wao Manchester United, ingawa amesema hatomsajili mbadala wake, kwani tayari alishapata kabla ya kumruhusu. 
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kukubaliana ada ya uhamisho na United, Wenger alisema: “Ni huzuni kubwa unapopoteza mchezaji wako bora kama yeye. Alibakisha mwaka mmoja kwenye mkataba wake, hivyo hatukuwa na chaguo zaidi.”
Alipoulizwa kama atatumia kiasi cha pesa alichovuna kumuuza mkali huyo kusajili wachezaji wapya, Wenger alijibu: “Tayari tulishapata wa kujaza nafasi yake kabla ya kumruhusu na sitarajii kusajili yeyote wa kumrithi, ninao kikosini.”
Katika taarifa ya klabu kwenye tovuti, Gunners ilisema: “Van Persie atasafiri kwenda Manchester leo Alhamisi, kwa ajili ya makubaliano binafsi, ikiwamo vipimo vya afya ili kumalizia hatua zilizosalia za uhamisho wake.”
Kwa upande wake Msemaji wa United aliongeza: “Tuna furaha kutangaza kuwa, tumekubaliana na Arsenal kwa ajili ya uhamisho wa Robin Van Persie kuja Man United.”
Aidha kocha Sir Alex Ferguson, ametambia usajili wa Van Persie ulioigharimu klabu yake pauni milioni 22, huku nyota huyo akiahidi ushambuliaji pacha tishio utakaobeba tija na nyota wa Manchester United, Wayne Rooney.
Van Persie aliyekuwa nahodha wa Arsenal, jana alikuwa Old Trafford yaliko makazi ya Man United, kwa ajili ya vipimo vya afya yake, ikiwamo makubaliano binafsi ya mshahara wake unaotarajiwa kuwa zaidi ya pauni 200,000 kwa wiki.
Taarifa za kukubali kwa Gunners kumruhusu Mholanzi huyo kujiunga na United zilitolewa juzi, ambapo Fergie alisema ana matumaini makubwa ya kumaliza kila kitu kuhusu mkali huyo kufikia wikiendi hii.
Van Persie, 29, ambaye alikataa kurefusha mkataba wake na Arsenal, alimwambia kocha huyo Mskochi kuwa yu tayari kutumika kama pacha wa mbele au nyuma ya Rooney na kwamba atakuwa na ushirika mwema.
Kukubaliwa kwa dau la United kupata saini ya RVP kulipokelewa kwa furaha na Rooney, aliyeingia kwenye kurasa ya ‘twitter’ na kumtania shabiki maarufu wa Arsenal aitwaye Piers Morgan.
Akaandika kwenye ukurasa huo: “Arrrr, maskini Piers. Uhalia gani kwa sasa, mkubwa?”, ambapo bila kusita Morgan akaujibu ujumbe huo kwa kumuita Rooney “mshambuliaji namba mbili klabuni Old Trafford.”

No comments:

Post a Comment