Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF Prof. Ibrahim Lipumba.
Na.Mwandishi wetu.
Chama
cha Wananchi (CUF) kimelaani mauaji ya Mwandishi wa habari wa kituo cha
Channel Ten, Daudi Mwangosi huku kikimtaka Rais Jakaya Kikwete kubeba
jukumu hilo ikiwa ni pamoja na kuunda Tume huru.
Katika
tamko lao jijini Dar es Salaam, lililotolewa na Mwenyekiti wake Prof.
Ibrahim Lipumba, Rais Kikwete anapaswa kuunda Tume hiyo ambayo
itawashirikisha Watetezi wa Haki za Binadamu, Madaktari, Wakuu wa Jeshi
la Polisi na Upelelezi pamoja na Wajumbe wengine wa vyama vya siasa.
Kwa
mujibu wa Lipumba Tume ya Rais iwe na jukumu kubwa moja la kuchunguza
mauaji hayo ambayo taarifa zake zinatatanisha hadi sasa, kwa lengo la
kupata ukweli utakaofanyiwa kazi ya kukomesha mauaji yasiendelee
kutokea.
Aidha
kwa upande wa Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA), limelaani tukio
hilo na kusema pindi uchunguzi utakapokamilika na kubainika ukweli,
basi wahusika wote wawajibishwe na wabebeshwe jukumu la kulipa fidia kwa
familia ya marehemu.
Pia
TUCTA, imelishauri jeshi la polisi katika kubuni mbinu mpya za kisasa
ili kukabiliana na vurugu zinazotokana na harakati za kisiasa, kwani
kuamini katika matumizi ya silaha pekee kamwe hakuwezi kuwa suluhisho la
vurugu, matokeo yake ni kujenga usugu kwa Wananchi na matokeo yake
hayatakuwa mazuri.
No comments:
Post a Comment