Wednesday, September 26, 2012

TANZIA; MWANDISHI TANZANIA DAIMA AFARIKI DUNIA LEO



DAR ES SALAAM, Tanzania
MWANDISHI wa habari wa Kampuni ya Free Media Ltd inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Agnes Yamo, amefariki dunia alfajiri ya leo kwenye Hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Habari Mseto, Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima, Absalom Kibanda, amesema familia ya marehemu Agnes imethibitisha kutokea kwa msiba huo na kuwa marehemu amekufa wakati akipata matibabu kutokana na upungufu wa damu.
Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), aliongeza kuwa msiba wa Agnes uko nyumbani kwa kaka yake Buguruni Sokoni (Rozana) kwenye mafleti ya Muhimbili.
Enzi za uhai wake, Agnes aliyezaliwa Agosti 9, 1978, alikuwa mwandishi aliyefanya kazi Kampuni ya Habari Corporation, kabla ya Tanzania Daima alikofanya uandishi kwa muda na baadaye kugeukia Idara ya Matangazo ya Free Media Ltd inayochapisha gazeti hilo, hadi umauti ulipomkuta.
Kwa mujibu wa Kibanda, mipango ya mazishi inaendelea kufanyika nyumbani kwa kaka wa marehemu, ambapo mwili unatarajiwa kusafirishwa kesho Jumatano jioni kwenda Morogoro yatakakofanyika maziko yake.
Shughuli za kutoa heshima za mwisho na kuuaga mwili wa marehemu zinatarajiwa kufanyika nyumbani hapo kwa kaka yake Buguruni, kabla ya kusafirishwa. Mungu ailaze ROHO ya marehemu mahali pema PEPONI. Ameeeeeen

No comments:

Post a Comment