Sunday, October 28, 2012

CUF YAZINDUA KAMPENI ZA UDIWANI MKOANI MOROGORO



Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Mtibwa, Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro. (Picha na Salmin Said, OMKR)


MOROGORO, T anzania
Chama Cha Wananchi CUF kimesema kuwa kinakusudia kujenga uchumi imara utakaoweza kumnufaisha kila Mtanzania popote alipo bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza hayo wakati akifunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kwa chama hicho katika kata ya Mtibwa, Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.

Amesema Watanzania bado hawajanufaika ipasavyo kutokana na rasimali zake zikiwemo ardhi, madini na wataalamu, hali inayotokana na mfumo wa uongozi usiozingatia mgawano wa rasilimali za nchi kwa maslahi ya wananchi.

“Mimi nashangaa sana, kwa nini serikali ya Tanzania inashindwa kumtumia Prof. Lipumba, wakati nchi nyengine za Afrika Mashariki na jumuiya za kimataifa zinamtumia vizuri kukuza uchumi wa nchi na taasisi hizo”, alihoji Maalim Seif.

Amefahamisha kuwa CUF ni chama chenye sera za kumkomboa mtanzania, na kuwaomba wananchi wa mkoa huo kukiunga mkono ili kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi katika eneo hilo na mikoa mengine ya Tanzania.

“Wananchi tunahitaji kuleta mabadiliko ya msingi katika nchi yetu, tatizo tulilonalo sasa ni viongozi wasiokuwa na dira ya mabadiliko”, alifahamisha.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa haki za binadamu, uenezi, mawasiliano na umma wa Chama hicho Bw. Abdul Kambaya amesema wananchi wa kata ya Mtibwa wana kila sababu ya kuleta mabadiliko ya uongozi katika eneo hilo kutokana na manufaa madogo wanayoyapata licha ya kuwa na rasilimali zilizowazunguka.

“Sukari kwa mfano, inazalishwa katika kata hii ya Mtibwa lakini wananchi wa Mtibwa munanunua sukari kwa bei sawa sawa na wanavyonunua wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, kulikoni”? alihoji Kambaya.

Amefahamisha kuwa wananchi wa eneo hilo pia wamekuwa wakikosa msingi bora wa elimu kutokana na ukosefu wa walimu unaotokana na mfumo mzima wa elimu na uongozi unaolenga kuwanufaisha zaidi watoto wa viongozi.

“Sijui kuwa yupo mtoto wa Waziri, Katibu Mkuu au Mkurugenzi anaesoma katika skuli hii, ndio maana hamuendelei na munaishia darasa la saba, mutapataje ajira kwa elimu ya darasa la saba wakati huu, wao watoto wao wanawasomesha katika ‘International Schools’ hadi kumaliza madigrii yote, nyinyi mmelala tu munajisahau baada ya kufurahishwa kwa nyimbo za wasanii”, alifahamisha.

Kabla ya mkutano huo wa kufunga kampeni za udiwani, Maalim Seif alizungumza na wazee wa CUF wa Mkoa wa Morogoro, na kuwashukuru kwa kuendelea kukiunga mkono chama hicho.

“Nashkuru kuwa kwa muda wote huo hamkuyumba na hamkubali kuyumbishwa katika kutetea chama chenu, nakushkuruni sana kwa msimamo wenu huo”, aliwapongeza.

Nao wazee hao ambao kwa kiasi kikubwa wanajishughulisha na kazi za kilimo, wameelezea masikitiko yao ya kuhujumiwa kwa kilimo chao na wafugaji, jambo ambalo limekuwa likizorotesha maendeleo yao.

Wamemshukuru Katibu Mkuu huyo wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kwa kufika katika eneo hilo na kubadilishana mawazo juu ya changamoto mbali mbali zinazowakabili, na kuelezea kufarajika kwao kutokana na ujio wake.

No comments:

Post a Comment