Thursday, December 27, 2012

MADABIDA ALIVYOWAPA SOMO TAMPRO JIJINI DAR.


MWANASIASA mkongwe nchini Alhaj Ramadhan Rashid Madabida pichani juu, ameishauri Jumuiya ya wanataaluma wa Kiislamu nchini TAMPRO kuweka uwanja tambalale ili kuwawezesha vijana wasomi wa Kiislamu kupata mwelekeo wa kimasomo na kimaisha kwa lengo la kujenga ufanisi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla wake.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa asasi hiyo isiyo ya kiserikali uliyofanyika kwa siku mbili mfululizo jijini Dar es Salaam, Alhaj Madabida alisema Tampro kwa kuwatumia wataalamu wao, inaweza kuanzisha kambi za vjana wenye vipaji  maalum na kuwapa miongozo itakayowasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali katika masomo yao.
“TAMPRO mnaweza kuandaa kambi za vijana hasa wale walio kidato cha tano na sita na mkawashauri mbinu na mikakati rafiki itakayowawezesha kufanya vizuri katika masomo yao, kuliko kuwaacha kila mtu na lwake”, alisema Madabida.
Aidha Madabida ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam aliwapongeza wanachama wa TAMPRO kwa upande wa kwanza na viongozi wake kwa upande mwingine kwa kufanikiwa kukisimamisha chombo hicho ambacho alidai matunda yake yameanza kuonekana.
“Ingawa mnakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba wapo wanaobeza jitihada zenu katika kutelekeza malengo mliojiwekea, lakini ukweli unabaki palepale kwamba uwepo wa TAMPRO  ni faraja kwa jamii ya Waislamu hapa nchini”, alisema.
Akaongeza kuwa, uwepo wa taasisi hiyo ya wasomi ni faraja kwa jamii kwasababu inaonesha jinsi vijana wa Kiislamu wanavyojitambua juu ya wajibu wao katika kupeleka mbele maendeleo ya dini yao.
Naye Amir wa TAMPRO Mussa Mzia ameitaka jamii ya waislamu kuipa ushirikiano jumuiya hiyo katika harakati zake kwa kuwa moja ya malengo yake ni pamoja na kuihamasisha jamii hiyo katika kujiendeleza kielimu na kujiletea maendeleo.
Aidha Mzia akasema TAMPRO kama jumuiya ya wasomi wa Kiislamu, ina jukumu la kuwaunganisha wataalamu wote wa dini hiyo na kujenga umoja na mshikamano baina yao na hivyo akatoa wito  kwa wasomi wa kujiunga na asasi hiyo ili kutimiza malengo waliojiwekea ya kuanzisha miradi ya maendeleo  katika jamii ili jamii iweze kujifunza kutokana na miradi hiyo.

No comments:

Post a Comment