Wednesday, December 12, 2012

WALIOPATA DAWA YA BABU LOLIONDO WAZIDI KUPOTEZA MAISHA.




 Mchungaji Amilikile Masapila-Loliondo.

Kwa ufupi
Masinde alisema idadi ya vifo vilivyotokana na Ukimwi katika wilaya hiyo katika kipindi hicho, vimeongezeka kwa asilimia mbili ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
IDADI ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi katika Wilaya na Mkoa wa Geita, inasemekana imeongezeka katika kipindi cha mwaka 2011/12 kufuatia hatua ya baadhi ya wagonjwa, kuacha kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi baada ya kwenda Loliondo kwa babu na kupata kikombe cha dawa.

Hali kadhalika kuwapo kwa shughuli za migodi ya wachimbaji wadogo na uvuvi katika Ziwa Victoria, kumechangia ongezeko la vifo vya watu kutokana na ugonjwa huo.

Imeelezwa kuwa ongezeko la shughuli za kiuchumi katika maeneo ya madini na uvuvi, ni changamoto kubwa kwa idara ya afya wilayani humo  katika kupambana na kasi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi kwa wakazi wa Geita.


Mratibu wa Mpango wa Kudhibiti Ukimwi katika Wilaya ya Geita, Patrisia Masinde, aliiambia Mwananchi jana kuwa katika kipindi cha kati ya  Januari na Novemba mwaka huu, watu 31 walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo ambao hadi sasa haujapata tiba. 

Alisema watu hao ni  sehemu ya watu 131,waliokuwa wamelazwa katika vituo vya afya wakipata huduma.

Masinde alisema idadi ya vifo vilivyotokana na Ukimwi katika wilaya hiyo katika kipindi hicho, vimeongezeka kwa asilimia mbili ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, katika kipindi hicho mwaka jana, watu waliopoteza maisha kwa ugonjwa huo walikuwa 16.

Kwa upande wake, Mratibu wa Ukimwi katika Kitengo cha Matibabu katika Wilaya ya Geita, Dk.John Mgosha alisema vifo hivyo vinatokana na baadhi ya wagonjwa waliokwenda kwa Babu wa Loliondo na kupata kikombe cha dawa, kuacha kutumia vidonge vya kuvumbaza virusi vya Ukimwi.

Alisema baadhi ya watu hao  Loliondo waliamini kwamba Mchungaji Amilikile Masapila, alikuwa na dawa ya kutibu ugonjwa wa Ukimwi licha ya kutambua kuwa hakuna dawa iliyothibitishwa na watalaamu wa afya kutibu ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment