Thursday, December 27, 2012

Wanataaluma Wa Kiislamu Nchini (Tampro) Kusaidia Wanafunzi Sekondari Za Kata


JUMUIYA ya wanataaluma wa Kiislamu nchini (Tampro), imesema kwa kushirikiana na taasisi nyingine, inaandaa mpango mkakati wa kuhakikisha inawasaidia vijana wanaosoma katika shule za sekondari za Kata ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho kama sehemu ya jitihada zao kwa jamii ya Watanzania.
Akizungumza kuhusu  maazimio ya mkutano mkuu wa jumuiya hiyo uliomalizika juzi katika hotel ya Lamada jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji Jumuiya hiyo Sadiki Gogo, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuridhika na utafiti ilioufanya na kubaini kuna haja ya wao kama wanataaluma kutafuta njia ya kuwasaidia vijana hao kimasomo.
 
”Tampro kupitia kliniki yake ya Elimu, iliomba na kupata kibali Wizarani cha kufanya utafiti katika shule kadhaa za sekondari za kata hapa nchini na kugundua kuwa zina uwezo wa kufanya vizuri iwapo zitasaidiwa katika baadhi ya nyanja” alisema Gogo
Akifafanua baadhi ya nyanja hizo, Mkurugenzi  huyo, alisema  pamoja na kuwapa mafunzo maalum walimu wa shule hizo na baadae kupeleka walimu wa kujitolea katika baadhi ya shule zitakazoonekana zina upungufu mkubwa.
 
Sambamba na mkakati huo ambao amedai unalenga kuisaidia serikali, Gogo alisema Tampro kupitia mkutano huo imeazimia kuanzisha vituo vya Elimu maalum pamoja na huduma nyinginezo kwa watu wenye mahitaji maalum kama vile ya ulemavu.
 
Aidha Mkutano mkuu huo umeazimia kushirikiana na wadau wengine nchini kuwekeza katika sekta ya Afya kwa madai kuwa bila ya kuwa na watu wenye afya zilizoimarika ,ni ngumu Taifa kufikia maendeleo ya kisiasa na kiuchumi.
 
Tampro ni Jumuiya isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 1994 na kusajiliwa rasmi serikalini Agost 22, 1997 ikiwa na malengo  mengi na mojawapo ni kufanya tafiti, kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalam katika maeneo mbalimbali  ya maendeleo ya jamii.

No comments:

Post a Comment