Tuesday, December 4, 2012

Waziri Mathayo, Nape kuwashuhudia Miyeyusho, Nassib PTA


Mabondia Francis Miyeyusho (kushoto) na Nassib Ramadhani watakaopigana Desemba 9


WAKATI mabondia Francis Miyeyusho na Nassib Ramadhani wakitarajiwa kupima uzito Desemba 8 kabla ya kuvaana kuwania ubingwa wa Mabara wa WBF, viongozi waalikwa watakaoshuhudia pambano hilo wamefahamika.
Promota wa pambano hilo litakalofanyika jijini Dar siku ya Desemba 9, Mohammed Bawazir aliiambia MICHARAZO, miongoni mwa viongozi hao waalikwa ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo.
Bawazir alisema mbali na Dk Mathayo, wengine waliothibitisha kushuhudia pambano hilo la uzani wa Bantam ni pamoja na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na Katibu wa Itikidi na Uenezi-CCM, Nape Nnauye.
"Hao  ni baadhi ya viongozi wakuu tuliowatumia mwaliko na kutuhakikishia watahudhuria na tutamtangaza mgeni rasmi siku ya Desemba 6," alisema.
Promota huyo alisema wangependa mgeni rasmi katika pambano hilo awe mmoja wa viongozi wa juu wa Taifa na ndiyo maana wanaendelea kusubiri majibu ya mwaliko wao kabla ya kumtangaza jina katika mkutano wao ujao.
Juu ya maandalizi ya pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kutokana na ubora na rekodi za mabondia hao wawili, Bawazir alisema yanaendelea vema japo wamekwama kupata wadhamini wa kuwapiga tafu.
Bawazir alisema pamoja na hayo bado wanaendelea kuitoa wito kwa watu wenye mapenzi mema na mchezo wa ngumi kujitokeza kuwapa nguvu, huku akisema upimwaji wa uzito na afya kwa mabondia utafanyika Desemba 8.
"Maandalizi yaendelea vema japo wadhamini wanasuasua kujitokeza na mabondia wote watapimwa kupimwa uzito na afya zao Desemba 8, siku moja kabla ya kupanda ulingoni," alisema.
Pambano hilo litafanyika chini ya usimamizi wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania, PST na litatanguliwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Michezo hiyo ya utangulizi ni kati ya Fadhili Majia vs Juma Fundi, Mohammed Matumla dhidi ya Doi Miyeyusho, Ibrahimu Class 'King Class Mawe' vs Said Mundi, Fred Sayuni dhidi ya Deo Samwel na Hassan Kidebe dhidi ya Baina Mazola.

No comments:

Post a Comment